Featured Kitaifa

SERIKALI MEZANI NA VYOMBO VYA USHAURI VYA UNESCO,WAJADILI KUHUSU MAENEO YA URITHI WA DUNIA

Written by mzalendoeditor

WAZIRI  wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro ameongoza timu ya wajumbe kutoka Tanzania waliohudhuria kikao cha pamoja na UNESCO katika Kituo cha Urithi wa Dunia kilichohusisha pia vyombo vya ushauri vya UNESCO yaani IUCN, ICOMOS na ICCROM. Kikao hicho kilifanyika tarehe 13 Julai 2022, Paris Ufaransa.

Katika kikao hicho, ujumbe wa Tanzania umeeleza na kujibu hoja mbalimbali zinazohusu hatua shirikishi za Serikali za kuwaomba na kuwalipa fidia jamii zilizokuwa zinaishi Ngorongoro kisha kuhamia kijiji cha Msomera Wilaya ya Handeni ili kuondoa changamoto za Uhifadhi wa eneo la Ngorongoro zilizosababishwa na uwepo wa idadi kubwa ya binadamu na mifugo ndani ya eneo la hifadhi, hatua ambayo itaboresha Ikolojia ya eneo hilo na Utalii.

Kwa upande wa Mji Mkongwe wa Zanzibar mazungumzo yalijikita katika Uhifadhi na Maendeleo bila kuathiri Urithi wa Utamaduni. Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro na Mji Mkongwe wa Zanzibar ni miongoni mwa maeneo Saba ya Tanzania kwenye Orodha ya Urithi wa Dunia unaolindwa na Mkataba wa UNESCO wa 1972.

Dkt. Ndumbaro amekitaarifu kituo cha Urithi wa Dunia cha UNESCO kuwa Tanzania imefanya kila jitihada kulinda maeneo hayo ya urithi wa Dunia kwa kuzingatia maelekezo ya Mkataba wa UNESCO wa Urithi wa Dunia wa 1972 pamoja na Sheria za ndani ya nchi yetu na za kimataifa. Aidha, Dkt. Ndumbaro amebainisha changamoto zinazojitokeza ni kutokana na upotoshaji unaofanywa ili kuwapotosha wananchi na kuchelewesha utekelezaji wa mipango ambayo ina maslahi mapana kwa wananchi husika, nchi yetu na dunia kwa ujumla.

Ujumbe wa Tanzania pia umepokea ushauri wa kituo cha UNESCO cha Urithi wa Dunia na majadiliano yanaendelea juu ya namna bora ya kulinda na kuhifadhi Urithi wa Dunia.

Pamoja na Waziri Mhe. Ndumbaro, Serikali ya Tanzania imewakilishwa na Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Prof. Eliamani Sedoyeka, Katibu Mkuu Wizara ya Urithi na Utalii Zanzibar, Bi. Fatma Mabrouk Khamis, Mh. Balozi Samuel Shelukindo ambae ni Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa na Mwakilishi wa Kudumu UNESCO.

Aidha walikuwepo Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya UNESCO ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Prof. Hamisi Malebo na Bw. Erick Kajiru, Afisa Programu Mkuu katika Tume ya Taifa ya UNESCO ambaye pia ni Mratibu wa Masuala ya Urithi wa Dunia nchini. Wengine katika ujumbe wa Tanzania ni Kaimu Mhifadhi Mkuu wa NCAA Dkt. Christopher Timbuka, Bw. Joshua Mwankunda ambae ni Mhifadhi Mwandamizi wa NCAA na Mhandisi Musa Aweso kutoka Mamlala ya Mji Mkongwe wa Zanzibar.

Kwa upande wa UNESCO iliongozwa na Ndg. Lazare Eloundou Assomo, Mkurugenzi wa Kituo cha Urithi wa Dunia, UNESCO

About the author

mzalendoeditor