Featured Kitaifa

SAGINI AMSHUKURU RAIS SAMIA KWA MIRADI YA MAENDELEO BUTIAMA, AHIMIZA KUSHIRIKI SENSA YA WATU NA MAKAZI.

Written by mzalendoeditor

Mbunge wa Jimbo la Butiama, Jumanne Sagini akikagua Mradi wa Maji uliopo katika Kijiji cha  Nyasirori, Kata ya Masaba na wa Kijiji cha Mwibagi ikiwa ni sehemu ya ziara yake jimboni kwake Butiama.

Mbunge wa Jimbo la Butiama, Jumanne Sagini akikagua Miradi ya Ujenzi wa Zahanati wa Kijiji cha Kwigutu, Kata ya Masaba na wa Kijji cha Magunga , Kata ya Mirwa ikiwa ni sehemu ya ziara yake jimboni kwake Butiama.

Mbunge wa Jimbo la Butiama akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Mwibagi, kata ya Kyanyari kwenye moja ya Mikutano yake ya hadhara, Butiama.

……………………………………….

Na mwandishi wetu,

Mbunge wa Jimbo la Butiama mkoani Mara, Jumanne Sagini amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kufanikisha miradi mbalimbali ya maendeleo hususani katika sekta za elimu, maji, afya na miundombinu ya barabara ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Butiama.

Akizungumza na wananchi wa Jimbo la Butiama, Sagini amesema kuwa Serikali ya Awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia inaendelea kutekeleza mipango ya maendeleo na kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma stahiki zitakazosaidia kupunguza changamoto wanazokumbana nazo katika shughuli zao.

“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuleta miradi yenye nia njema ya kuleta maendeleo kwa Watanzania, niwaombe mtumie fursa hii kwa kufanya kazi kwa bidii ili nchi yetu izidi kuendelea” amesema.

Sagini alisema hayo wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Masaba, Buruma, Mirwa, Kyanyari na Kukirango kwa nyakati tofauti baada ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika kata hizo ikiwa ni sehemu ya ziara yake mkoani Mara.

Akitoa salamu za Rais Samia, Sagini amewataka wananchi wa Jimbo la Butiama na watanzania kwa ujumla kujiandaa kushiriki katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika Kitaifa tarehe 23 Agosti 2022.

Amesema kuwa Sensa ya watu na makazi inasaidia Serikali kupata idadi ya watu inayo saidia upangaji wa mipango ya maendeleo nchini.

“Mimi Mbunge wa Jimbo la Butiama nipo tayari kushiriki kwenye Sensa ya Watu na Makazi, niwaombe watanzania wa Butiama kujitokeza Agosti 23. Ukihesabiwa ukajulikana ndio huduma za kijamii na za kiuchumi zitapangwa na kutolewa”

Katika hatua nyingine Mbunge Sagini ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi amewataka waendesha bodaboda kutii Sheria za Usalama Barabarani na kuepuka kufanya vitendo vya uhalifu vitakavyowapelekea kuwa wateja wa Jeshi la Polisi.

“Kazi ya Kikosi cha Usalama Barabarani ni kulinda usalama wa waendesha vyombo vya moto pamoja na abiria. Ukisimamishwa niwaombe msikimbie”

About the author

mzalendoeditor