Featured Kitaifa

WANASAYANSI KUTOKA MATAIFA 50 WAKUTANA ARUSHA KUJADILI NAMNA YA KUTUMIA PANYA KATIKA UDHIBITI WA MABOMU

Written by mzalendoeditor
Mwenyekiti wa mkutano huo, ambaye ni Mtaalamu wa Utafiti wa Ikolojia ya Panya kutoka Kituo cha Umahiri cha Utafiti wa Panya cha Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Prof. Rhodes Makundi akiongea na waandishi wa habari 
………………………………………….
NA NAMNYAK KIVUYO, ARUSHA 
Wanasayansi na watafiti wa panya kutoka nchi zaidi ya 50 duniani, wamekutana  Jijini Arusha, kujadili namna ya kuwatumia Panya katika udhibiti,kugundua mabomu na kugundua maambukizi ya ugonjwa wa tauni na uokozi wa majanga ya kidunia.
Aidha katika  mkutano huo wa saba wa kimataifa wa baiolojia ya panya na udhibiti wa panya duniani unaofanyika jijini Arusha,Tanzania imeishangaza dunia, baada ya kufanikiwa kugundua na kuwafundisha panya tisa wa uokozi, kutambua majeruhi na watu waliopoteza maisha katika ajali, hasa kwenye majengo.
Mwenyekiti wa mkutano huo, ambaye ni Mtaalamu wa Utafiti wa Ikolojia ya Panya kutoka Kituo cha Umahiri cha Utafiti wa Panya cha Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Prof. Rhodes Makundi, amesema kuwa ,watafiti hao wanaangalia mambo tofauti tofauti, kwanza wanaangalia kitu kinachoitwa taxonomy (utambuzi panya wako wa aina gani), pili biodiversity (katika mazingira wanayoishi, kwamba kuna wanyama gani na wanahusianaje),na kingine ni juu ya magonjwa yanayotukabili kutokana na panya.
“Pia, tunaangalia udhibiti wa panya, kwa kutumia njia za kiikolojia, tunaangalia tabia za panya, tunaangalia panya wanaopatikana katika Milima na Mabonde katika Afrika, hasa katika nchi za Afrika ya Mashariki.”amesema Prof.Makundi.
 Ameongeza kuwa , kingine ni kuangalia matumizi ya panya ili kuleta faida kwa jamii; kwa mfano matumizi ya panya kwenye kugundua mabomu, kugundua ugonjwa wa tauni na mambo mengine, ambayo panya anaweza akatumika.
Prof. Makundi, amesema kuwa, baada ya mkutano huo wanatarajia, jopo la Wanasayansi hao ambao wamefanya utafiti kwenye nchi tofauti, hasa kudhibiti panya, Wanasayansi wa Tanzania, watajifunza mambo yanayofanyika katika nchi zingine , na pale inapowezekana utaalamu huo watauchukua kuutumia hapa nchini kutatua matatizo ya panya.
“Kwa mfano, utafiti wa matumizi ya panya kwenye kugundua kutegua mabomu, kugundua magonjwa ya tauni. Unaweza kuona utafiti huo unatumika nchi nyingi kama Cambodia huko.”amesema Prof .Makundi.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongela, akifungua mkutano huo amesisitiza kuwa kwa sasa umefika wakati, wanasayansi na watafiti hao, kutoka hadharani kuelezea zaidi faida ya eneo hilo ili lisibaki tu kuwa eneo la utafiti.
“Nawaomba sana wanasayansi wetu watoke sasa kueleza faida zake ili jamii ielewe zaidi juu ya faida za hili, kwa sababu tunaona kuna hasara nyingi kwenye upoteaji wa mazao na vyakula.”amesema .
“Wataalamu wetu, Wanasayansi wetu kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine, SUA, ndio ambao wanaendesha kwa kiwango kikubwa mkutano huu. Wanasayansi wengi duniani, ambao wako kwenye eneo hili la kutizama athari na faida za panya, “amesema Mongela.
 Mongela amesema kuwa,mkutano huo ni wa kipekee Sana kwani wanatizama athari wanazoweza kusababisha panya pamoja na faida, kwa sababu ni viumbe ambao ni muhimu kwa maendeleo, na watatizama maeneo yote kimaendeleo, kijamii na kisayansi.
“Wamekuja wanasayansi wabobezi wakubwa wanashiriki hapa, kwa hiyo hili mimi naliona kubwa sana kwa nchi yetu, kwanza kutambulika kwamba tuna kituo cha umahiri lakini, wanasayansi hawa wote wa dunia, kuja kwetu kutambua nafasi ya wanayasansi wetu wa Tanzania na kubadilishana ujuzi na machapisho mbalimbali na kazi za kisayansi za dunia nzima ambazo zinafanyika kwenye eneo hili, hasa utafiti wa panya.”amesema Mongela.
Mtafiti kutoka Shirika la Uhisani la APOPO linalojishughulisha na maisha ya panya, lililopo chini ya SUA, Venance Kiria, amesema kuwa, shirika hilo limewafundisha panya tisa wa uokozi, ambao mpaka sasa wako kwenye hatua ya mwisho katika ufundishaji.
 “Hivi sasa panya wa Tanzania, wana uwezo wa kutafuta mtu akiwa umbali mrefu, lakini si kwa kiwango kile ambacho tunakitaka, na hasa kwenye majengo yaliyopata ajali.”amesema Kiria.
 Ameongeza kuwa,  kwa  jinsi hali ilivyo sasa kuna ajali nyingi zinatokea sasa hivi kama majengo makubwa ya ghorofa kubomoka, kwa hiyo mojawapo ya manufaa mbalimbali zinazotokea baada ya hayo majengo kubomoka ni watu kupoteza maisha na wengine kujeruhiwa, lakini wanashindwa kutoka wakisubiri juhudi zetu ili tuweze kuwaokoa wao.”

About the author

mzalendoeditor