Featured

RC MTAKA ATAKA MAAFISA ARDHI KUACHA DHURUMA

Written by mzalendoeditor

MKUU wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka,akizungumza katika kikao cha kuwajengea uwezo  watendaji wapya na wale wazamani wa idara ya Ardhi kilichofanyika Jijini Dodoma.

Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini Jabir Shekimweri ,akizungumza kwenye  kikao cha kuwajengea uwezo  watendaji wapya na wale wazamani wa idara ya Ardhi kilichofanyika Jijini Dodoma.

Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru,akielezea mikakati ya jiji hilo kumaliza migogoro ya ardhi wakati wa  kikao cha kuwajengea uwezo  watendaji wapya na wale wazamani wa idara ya Ardhi kilichofanyika Jijini Dodoma.

Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma Prof.Davis Mwamfupe,akizungumza kwenye  kikao cha kuwajengea uwezo  watendaji wapya na wale wazamani wa idara ya Ardhi kilichofanyika Jijini Dodoma.

……………………………..

Na Eva Godwin-DODOMA

MKUU wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka amewataka baadhi ya Maafisa Ardhi kuacha dhuruma na badala yake wamrudie Mungu kwa kwenda kuwahudumia wananchi kwa haki bila upendeleo

Pia amewataka Maofisa wa idara hiyo waliohamishiwa Jijini Humo kwenda kutatua migogoro ya Ardhi kwa Wananchi na kwamba hicho ndicho kitakuwa kipimo cha utendaji wao wa kazi.

Mtaka ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama Mkoa wa Dodoma, ametoa agizo hilo wakati alipokuwa akizungumza na watendaji wapya na wale wazamani wa idara ya Ardhi kwenye kikao cha kuwajengea uwezo Jijini Dodoma.

” Baadhi ya wataalamu wa Idara ya Ardhi Jijini Dodoma wametengeneza migogoro mingi kwa wananchi kwa kutoa hati ya kiwanja kimoja kwa watu Zaidi ya wawili, huku wakiwapangia nini cha kufanya kwenye maeneo yao”,amesema

“Unakuta mtu ana shamba lake wapimaji wanakwenda kupima kisha wanamuondoa pale wanamwambia hapa kapewa mtu mwingine na mhusika atatafutiwa sehemu nyingine, nyie nyie hebu muogopeni Mungu vilio vya wananchi hawa ukivisikiliza vianakuumiza sana, fikiri kama shamba hilo lingekuwa la baba au babu yako ungemfanyia vitendo kama hivyo au ndiyo mkuki kwa Nguruwe kwa binadamu mchungu?”.Amesema Mtaka

Kwa Upande wake Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma Prof.Davis Mwamfupe,amesema kuwa mara nyingi amepokea malalamiko toka kwa wananchi kuwa wamejibiwa kuwa Mafaili hayaonekani na anapomuita mhusika anabaki akiwafokea.

“Tuambieni ukweli tu Mtu anapojibiwa kuwa faili lake halionekani maana yake kiwanja hicho kipo sokoni kinatafutiwa mtu mwingine auziwe na ndiyo sababu ya kiwanja kimoja kumilikiwa na watu Zaidi ya mmoja”,amesema.

“Mara nyingi nilipoletewa kesi ya namna hiyo nikimwita mhusika akijiumauma kwenye majibu huwa namwambia aniandikie kimaandishi kuwa faili la fulani halionekani, atakwambia ngoja nikajaribu tena baadae anakuja nalo na kusingizia kuwa lilikuwa lilichanganywa kwenye ofisi nyingine”.Amesema Mwamfupe

Naye Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini Jabir Shekimweri amesema ili kukomesha migogoro hiyo na kuondoa ubabaishaji katika uuzaji wa viwanja jiji hilo liweke kwenye mfumo wa Kidigital kila kitu kinachoihusu idara ya ardhi pamoja na orodha ya wamiliki na waombaji wapya.

Awali Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru, amesema makampuni ya upimaji yalichangia migogoro hiyo na kulitia jiji hasara kutokana na kupima viwanja vidogo kwa lengo la kupata viwanja vingi ili waweze kulipwa Zaidi.

“mfano unakuta eneo ni la kupima ukubwa wa mita za mraba 2000 au Zaidi wao wanapima ukubwa Square Mita 600 au 800, ili walipwe fedha za viwanja vingi lakini bila ufanisi, hivyo tangu sasa hatutatumia makampuni ya upimaji”,amesema.

“Tumenunua vifaa vya kupimia Zaidi ya 40 mil. Na magari matatu kwa ajili ya shuhuli za kupimia viwanja”.Amesema Mafuru

About the author

mzalendoeditor