Featured Kitaifa

‘WAZIRI MHAGAMA:’TASAF YABORESHA HUDUMA YA AFYA YA MAMA NA MTOTO MKOANI NJOMBE’

Written by mzalendoeditor

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akielezea azma ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ya kutoa fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kwa ajili ya kuboresha huduma za afya katika Mkoa wa Njombe.

Mwonekano wa jengo la afya ya mama na mtoto katika Mkoa wa Njombe linaloendelea kujengwa kupitia fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF)

Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Mhe. Kissa Kasongwa akielezea namna miradi ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) inavyowanufaisha wananchi wa Mkoa wa Njombe wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama iliyolenga kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika Mkoa wa Njombe.

Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), Bw. John Steven akielezea namna TASAF ilivyochangia kuboresha huduma za jamii katika sekta ya afya, elimu na miundombinu katika Mkoa wa Njombe wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama iliyolenga kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika mkoa huo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na Waratibu na Wahasibu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) Mkoa wa Njombe wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika mkoa huo.

Waratibu na Wahasibu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri huyo iliyolenga kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika Mkoa wa Njombe.

Mkurugenzi wa Halmashauri Wilaya ya Njombe, Bi. Sharifa Nabarangánya akielezea namna miradi ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) inavyowanufaisha wananchi halmashauri yake wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama iliyolenga kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika Mkoa wa Njombe.

Mratibu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) wa Halmashauri ya Mji Makambako, Bw. Regis Ngítu akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wa halmashauri hiyo kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri huyo iliyolenga kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika Mkoa wa Njombe.

…………………………………….

Na. James K. Mwanamyoto-Njombe

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amesema, Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) inajenga wodi ya afya ya mama na mtoto katika Hospitali ya Kibena iliyopo wilayani Njombe itakayoboresha huduma ya afya ya uzazi kwa akina mama ikiwa ni pamoja na kutunza watoto waliozaliwa kabla ya muda mkoani Njombe. 

Mhe. Jenista amesema hayo, wakati akikagua mradi wa ujenzi wa wodi ya afya ya mama na mtoto wilayani Njombe akiwa kwenye ziara ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF mkoani Njombe. 

“Jengo hili tulilolikagua leo ni wodi ya akina mama wanaojifungua, vilevile jengo hili limeandaliwa pia kwa ajili ya matunzo ya watoto ambao wamezaliwa kabla ya muda maalum kama watoto njiti,” Mhe. Jenista amefafanua.

Akizungumzia idadi ya miradi ya TASAF mkoani Njombe, Mhe. Jenista amesema, Mkoa wa Njombe una miradi 54 ambayo imegawanyika katika halmashauri zote, na kuongeza kuwa, jambo la kufurahia ni kuwa miradi hiyo imelenga kutatua changamoto zinazowakabili wananchi katika sekta za elimu, afya na miundombinu ya barabara.

“Halmashauri za Wilaya ya Njombe, Makambako na Makete zilikuwa zikikabiliwa na changamoto kubwa ya upungufu wa madarasa katika shule za msingi na kuna maeneo yalikuwa na shule shikizi hivyo kuwalazimu watoto wa shule kutembea umbali mrefu kwa ajili ya kuhudhuria masomo, lakini Serikali kupitia maono ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ya utekelezaji wa miradi ya TASAF imefanikiwa kutatua changamoto zote hizo,” Mhe. Jenista amesisitiza.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Mhe. Kissa Kasongwa amesema kuwa jengo hilo la afya ya mama na mtoto ambalo litatumika pia kuhifadhi watoto wanaozaliwa kabla ya muda litatatua changamoto kubwa ya huduma hiyo iliyokuwa ikiwakabili wananchi katika wilaya yake.

“Wananchi wilayani Njombe waliposikia Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kupitia TASAF ametoa shilingi milioni 92 kujenga jengo hili la afya ya uzazi kwa akina mama, nao walichangia shilingi milioni 11 ndani ya wiki moja ili kuunga mkono jitihada za Mhe. Rais za kuboresha huduma katika sekta ya afya,” Mhe. Kasongwa ameeleza.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, Bi. Sharifa Nabarang’anya amesema, wananchi wake wanamshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutatua changamoto zilizokuwa zikiwakabili kwenye sekta ya afya, elimu na miundombinu, akiainisha kuwa kuanzia mwezi Machi mwaka huu, halmashauri yake imepokea jumla ya shilingi milioni 495 kwa ajili ya kujenga zahanati tatu ambazo zitakamilika tarehe 30 Agosti, 2022 na kuanza kutoa huduma kwa wananchi.

Aidha, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Njombe, Bi. Kuruthum Sadick amemshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuleta miradi mikubwa inayoboresha huduma za kijamii kwa wananchi, hususan mradi wa ujenzi wa jengo la afya ya mama na mtoto ambao utatoa huduma kwa akina mama wengi wa Mkoa wa Njombe. 

Akimuwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Bw. John Steven ambaye ni Mkurugenzi wa Miradi TASAF amesema kuwa, ameambatana na Waziri Jenista Mhagama kwa ajili ya kukagua miradi ya TASAF inayofadhiliwa na Shirika la Uzalishaji Mafuta Duniani (OPEC) ambayo itatekelezwa mpaka mwaka 2025 mkoani Njombe.

Jumla ya miradi 54 ya TASAF mkoani Njombe inafadhiliwa na Shirika la Uzalishaji Mafuta Duniani (OPEC). 

About the author

mzalendoeditor