Featured Kitaifa

VIJJANA WASHAURIWA KUJIUNGA NA KOZI ZA UZALISHAJI WA SUKARI

Written by mzalendoeditor

NA MWANDISHI WETU: MOROGORO

Wito umetolewa kwa vijana kote nchini  kujiunga na kozi ya Teknolojia ya uzalishaji wa miwa na sukari ili waweze kuongeza chachu ya uzalishaji wa sukari kukidhi mahitaji ya soko la bidhaa hiyo nchini.

Wito huo umetolewa na Kaimu Mkuu wa Chuo Cha Sukari cha Taifa (NSI), Aloyce Kasmir, wakati alipozungumza na Mtandao wa Fullshangwe chuoni hapo, Kilombero Wilayani Kilosa Mkoani Morogoro jana.

 Kasmir amesema kuwa sekta ya sukari inakua kwa kasi kutokana na mahitaji  makubwa ya bidhaa hiyo kwenye soko la ndani na nje ya nchi, hivyo ukuaji huo unapaswa kwenda sambamba na ongezeko la wataalamu wenye ujuzi wa teknolojia bora na ya kisasa ya uzalishaji wa miwa na sukari.

“Kuna mahitaji makubwa ya wataalamu wa sukari kwa ajili ya kusaidia wakulima wa miwa waweze kuzalisha kwa mbinu bora na za kisasa sambamba na kuhudumia viwanda vya sukari.” Anasema Kasmir.

 Kasmir anaongeza kusema  kuwa serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, inavutia wawekezaji wa ndani na nje ya kuwekeza kwenye viwanda vya sukari sambamba na viwanda vilivyopo kuongeza uzalishaji, hivyo kupelekea mahitaji makubwa ya wataalamu wa sekta ya sukari. 

Kasmir anawashauri vijana kote nchini kujiunga na kozi za Teknolojia ya Uzalishaji wa Sukari (SPT) na kozi ya uzalishaji wa Miwa (SGP) kwa kuwa fani hizo zina fursa ya kupata ajira na  kuchochea ukuaji wa sekta ya sukari nchini. 

Akitaja sifa za kujiunga na chuo cha Taifa cha Sukari, Kasmiri alisema kuwa muombaji anapaswa kuwa amehitimu elimu ya sekondari Kidato cha nne na awe amefaulu masomo manne kwa alama D, kati ya hayo masomo mawili yawe ni masomo ya sayansi.

 

About the author

mzalendoeditor