Featured Kitaifa

CHUO KIKUU CHA MZUMBE KUFUNGUA TAWI TANGA

Written by mzalendoeditor

MKUU wa Mkoa wa Tanga Adam Malima akizungumza mara baada ya mazungumzo hayo
MKUU wa Mkoa wa Tanga Adam Malima  akiongoza kikao cha majadiliano ya
kuanzishwa kwa Kampasi ya Chuo cha Mzumbe Mkoani hapa na uongozi wa chuo
hicho
MKUU wa Mkoa wa Tanga Adam Malima akiongoza kikao cha majadiliano ya
kuanzishwa kwa Kampasi ya Chuo cha Mzumbe Mkoani hapa na uongozi wa chuo
hicho

 Serikali imetenga Sh bilioni 15 kwa ajili ya ujenzi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe mkoani Tanga.
Makamu
Mkuu wa chuo hicho, Profesa Lughano Kusihika amesema hayo wakati yeye
na ujumbe wake ulipokutana na Mkuu wa Mkoa wa Tanga kwa ajili ya
mazungumzo na kujadiliana eneo la kujenga chuo hicho.
Alisema
serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeamua kwamba
Chuo Kikuu cha Mzumbe kishiriki katika kuanzishwa kwa chuo kikuu katika
Mkoa wa Tanga na kwamba fedha kwa ajili ya shughuli hiyo ni mkopo wa
masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia (IMF) kwa ajili ya kuboresha
miundombinu na rasilimali watu na Mzumbe ni moja kati ya vyuo ambavyo
vimepata fursa hiyo.
“Kwa
ajili ya kuanzisha kampasi ya Tanga zimetolewa Sh bilioni 15 kwa hiyo
tuko katika maandalizi ya kufanya shughuli hiyo na sisi kama Mzumbe
tumefurahi kwa heshima ambayo tumepewa Mkoa wa Tanga ya kuja kuanzisha
kampasi yetu hapa.
“Mkoa wa
Tanga wote tunaufahamu ni mkoa mkubwa ambao una mambo mengi na huko
nyuma ulikuwa ni maarufu sana kwa ajili ya viwanda na wote tunajua
kwamba serikali yetu inataka kujenga uchumi wa viwanda, kwa hiyo sisi
ambao tuko katika vyuo vikuu tunatakiwa tushiriki kikamilifu katika
shughuli hii na mradi wenyewe kwa ujumla wake unafadhiliwa na IMF kwa
mageuzi ya kiuchumi,” alisema.
Alitaja
lengo kubwa la serikali ni kuangalia namna gani vyuo vikuu
vitashirikiana na jamii katika maeneo mbalimbali kuendesha programu na
kujenga uwezo kwenye maeneo hayo na kufanya shughuli ambazo zitaleta
mageuzi.
Profesa Kusihika
alisema bado wanaendelea na majadiliano ya kupata eneo ambalo wanaweza
kuanza ujenzi ambapo alifafanua zaidi lengo la serikali ni kuanzisha
kampasi na kuikuza halafu huenda huko mbeleni ikafika mahala ikawa ni
chuo kikuu kinachojitegemea.
“Kwa
hiyo tunawaomba sana wakazi wa Mkoa wa Tanga na viongozi wao, wapokee
hili wazo zuri kutoka serikalini kwa sababu lina maslahi makubwa na
mapana kwa nchi yetu maana sasa hivi serikali inafanya mapinduzi makubwa
katika mkoa huu ambapo inakwenda kuwekeza kwenye bandari pia tunajua
bomba la mafuta linalotoka Hoima litakuja kuingia Tanga.
“Hayo
yote yanaonyesha kwamba tutakuwa na shughuli nyingi za kiuchumi lakini
tunahitaji kuwatayarisha watu wetu ili waweze kushiriki katika kutumia
fursa hizo na maendeleo ya mkoa wa Tanga na Tanga ikiendelea inachangia
kwenye maendeleo yetu,” alisema Profesa Kusihika.
Awali,
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Adam Malima alisema wamefanya mazungumzo na
uongozi wa kujua wanafanya lakini fedha zimeshatoka kwa ajili ya
kuanzisha chuo kikuu hicho mkoani hapa.
“Tulichokunaliana
ni kwamba mwezi ujao Julai hadi Agosti, tutaanzisha Chuo Kikuu cha
Mzumbe hapa Tanga kwenye maeneo ya makazi ya muda wakati tunafanya
ujenzi wa makazi ya kudumu kwa sababu kuna maeneo matatu Mkinga, Muheza
na Tanga.
“Tulikuwa
tunajadiliana maeneo kwa sababu mwanzo ilikuwa fikra kwamba lipatikane
eneo la ekari kama 200 lakini ukipata ekari 200 leo baada ya miaka 20
utahitaji eneo la ekari 300-400 huna sehemu ya kupanua Tukasema hapana
ndiyo maana nimewaita wakuu wangu wa wilaya wa maeneo hayo, Mstahiki
Meya, Katibu Tawala na Ofisa Elimu wa Mkoa kwa sababu ni jambo ambalo
kimkakati kwa masaa haya yanayokuja tunataka tupate eneo ambalo wote
hapa tutaliangalia kwa pamoja,” alisema Malima.
Pamoja
na mambo mengine, Malima alisema walikuwa na mkutano na Katibu Mkuu wa
Mifugo wakakubaliana kutakuwa na Kitivo cha Mifugo ili kuendana na
mahitaji ya mifugo, Kitivo cha Mambo ya Uchumi wa Buluu na mambo mengi
ambayo bado wanawaza ili chuo kiwe kinafundisha masomo mahsusi ambayo
yanaendana na mahitaji ya kanda hiyo na maeneo mengine ya Tanzania kwa
ujumla.
“Tumekuwa na mkutano
mzuri ambao tunaamini kwa maamuzi haya Tanga sasa itapata chuo kikuu na
fikra ni kwamba baada ya miaka 10 kiwe ni chuo kikuu kinachojitegemea.
“Tunawashukuru
uongozi kwa kutufikiria sisi Tanga kwanza kama ni sehemu ya kuja kuweka
tawi lao nataka niwahakikishie Wanatanga kuwa huenda mwaka huu au
mwakani tutakuwa kwenye makazi ya muda miaka miwili tutakuwa kwenye eneo
mahsusi,” alisema.

About the author

mzalendoeditor