Featured Kitaifa

MKUTANO WA TANO WA JUKWAA LA TAIFA LA WADAU WA SEKTA MTAMBUKA KATIKA USIMAMIZI NA UENDELEZAJI WA RASILIMALI ZA MAJI

Written by mzalendoeditor

Wizara ya Maji kwa kushirikiana na Taasisi ya 2030 Water Resources Group, Global Water Partnership Tanzania na Ubalozi wa Canada wanaandaa Mkutano wa Tano (5) wa Jukwaa la Taifa la Wadau wa Sekta Mtambuka katika Usimamizi na Uendelezaji wa Rasilimali za Maji (National Multi-Sectoral Water Resources Management and Development Forum) utakaofanyika tarehe 18 Juni 2022 katika Ukumbi wa Mikutano wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), jijini Dar es Salaam. 

Madhumuni makuu ya Mkutano huu ni kupitia utekelezaji wa maazimio ya Mkutano wa Nne (4); kuidhinisha Hadidu za Rejea za vikundi kazi pamoja na kuzindua Mpango Mkakati wa Jukwaa; kubadilishana uzoefu wa kimataifa wa namna bora ya kushirikisha sekta mbalimbali katika usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji; kujadili mikakati na njia mbalimbali za kupata fedha katika kusimamia na kuendeleza rasilimali za maji.

Kauli mbiu ya mwaka huu ni: “Thamani ya Maji – Mchango wa Rasilimali za Maji Kwenye Uchumi wa Taifa” (The Value of Water – Contribution of Water Resources in the Country’s Economy).

Chimbuko la kuanzishwa jukwaa hilo linatokana na changamoto mbalimbali zilizotokana na uratibu usioridhisha wa sekta na taasisi mbalimbali, ongezeko kubwa la mahitaji ya maji pamoja na mabadiliko ya tabianchi. Aidha, uanzishwaji wa majukwaa haya ni kuongeza ushiriki wa wadau, hususan Sekta Binafsi na Washirika wa Maendeleo, katika usimamizi wa rasilimali za maji uliowekwa kisera na kisheria (Sera ya Taifa ya Maji, 2002 na Sheria ya Usimamizi wa Rasilimali za Maji Na. 11 ya mwaka 2009) katika kutekeleza Dhana ya Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Maji (Integrated Water Resources Management).

Mkutano wa Tano (5) wa Jukwaa hilo utafanyika tarehe 18 Juni, 2022 kuanzia saa 3:00 asubuhi katika Ukumbi wa Mikutano wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dar es Salaam na Mgeni Rasmi atakuwa ni Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb). 

Mkutano huo utatanguliwa na Kikao cha Kamati ya Uendeshaji ya Jukwaa hilo (Forum Steering Committee) na kikao cha Vikundi Kazi (Working Groups) ambavyo kwa pamoja vitafanyika tarehe 17 Juni, 2022 na kuandaa mpango kazi wa utekelezaji wa mwaka 2022/2033. Wadau wa rasilimali za maji wapatao 230 kutoka Wizara na Taasisi za Serikali, Taasisi zisizo za Serikali, Sekta Binafsi, Wadau wa Maendeleo, Vyuo Vikuu na Taasisi za Utafiti wanatarajiwa kushiriki mkutano huu.

Mhandisi Anthony Sanga

Katibu Mkuu

Wizara ya Maji

About the author

mzalendoeditor