Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Jumanne Sagini ambaye ni Mgeni Rasmi akiwasili katika Ufunguzi wa Mkutano wa Chama cha Sekta Binafsi ya Ulinzi Tanzania (TSIA) uliofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya New Dodoma Hotel, leo Juni 9, 2022.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Jumanne Sagini ambaye ni Mgeni Rasmi akizungumza na Wamiliki wa Kampuni ya Ulinzi walioshiriki katika Mkutano wa Chama cha Sekta Binafsi ya Ulinzi Tanzania (TSIA) uliofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya New Dodoma Hotel, leo Juni 9, 2022.
……………………………………………..
Na Mwandishi wetu,
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Jumanne Sagini amewataka wamiliki wa Makampuni Binafsi ya Ulinzi Tanzania kushirikiana na Jeshi la Polisi katika jukumu la kupambana na uhalifu hapa nchini.
Akizungumza na Wajumbe wa Chama cha Sekta ya Ulinzi Tanzania (TSIA) ambao pia ni wamiliki wa Makampuni Binafsi ya Ulinzi aliwaambia kuwa jukumu la kupambana na uhalifu hapa nchini sio la Jeshi la Polisi pekee ila ni la kila raia na kwamba sekta binafsi ya Ulinzi ni mdau mkubwa wa suala hili.
Aidha amewataka kutoa taarifa za uhalifu na kupeleka wahalifu hao Jeshi la Polisi endapo watawakamata.
“Ni mategemeo yangu kuwa mnapewa taarifa nyingi za uhalifu, mzifanyie kazi mara moja, aidha kuwakamata na kuwapeleka vituo vya Polisi endapo taarifa hizo zinahitaji huduma ya Jeshi la Polisi kwa ajili ya kufanyia kazi taarifa hizo zifikishwe Jeshi la Polisi”
Naibu Waziri Sagini aliyasema hayo leo wakati akifungua Mkutano wa Chama cha Sekta Binafsi ya Ulinzi Tanzania (TSIA) uliofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya New Dodoma Hoteli.
Naibu Waziri Sagini ameagiza silaha zote zitunzwe mahala salama na imara chini ya uangalizi wa watendaji wenye tabia njema na waaminifu. Amewataka kuzikagua silaha zao mara kwa mara na kuongeza umakini katika utunzaji wa silaha walizonazo kuepuka kufikia mikononi mwa wahalifu
“Silaha mahali salama ni jambo muhimu sana kwani mkizembea jambo hili mnaweza kuwa chanzo cha silaha zenu kuingia mikononi mwa watu wasio waaminifu hasa majambazi hivyo kuongeza tatizo la uhalifu nchini.”
Akiwapongeza kwa kwa kufanya Mkutano Mkuu wa Kumi na nne, Naibu Waziri Sagini amewataka kufanya tathmini ya maendeleo na changamoto za shughuli za chama chao na sekta binafsi ya ulinzi na kutumia fursa hii kujipima wapi walipokosea na hatua zitakazochukuliwa kurekebisha dosari hizo.
“Hii inaonyesha kwamba kuna uhai maana Chama hujengwa na kuimarika kwa wanachama kukutana na kujadili mambo ya maendeleo na mustakabali wa chama chao. Najua zipo changamoto mbalimbali kama zilivyoelezwa katika Risala yenu.”
Pia amewataka wamiliki wa Makampuni Binafsi ya Ulinzi Tanzania kuhakikisha kuwa walinzi wote wanakuwa na sare inayoweza kutambulisha walinzi wa kampuni, kutoa mafunzo ya weledi ya ulinzi, mafunzo ya kutumia silaha na kuanzisha kanzi data ili kuweza kutunza taarifa za wafanyakazi pamoja na kuratibu kazi.