Featured Kitaifa

WAZIRI MULAMULA ATOA WITO KWA JUMUIYA ZA KIKANDA KUSHIRIKIANA KATIKA KUTEKELEZA MAKUBALIANO YA AfCFTA

Written by mzalendoeditor

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akifungua Mkutano wa Pili (2) wa Uratibu wa Watendaji Wakuu wa Jumuiya za Kiuchumi za Kikanda (RECs) kuhusu utekelezaji wa Eneo Huru la Biashara la Afrika uliofanyika jijini Arusha.

Meza Kuu wakiwa tayari kushirikia Mkutano wa Pili (2) wa Uratibu wa Watendaji Wakuu wa Jumuiya za Kiuchumi za Kikanda (RECs) kuhusu utekelezaji wa Eneo Huru la Biashara la Afrika uliofanyika jijini Arusha. 

………………………………………..

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula ametoa wito kwa Jumuiya za kiuchumi za Kikanda za Afrika kushirikiana katika utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa kwenye Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA).

Waziri Mulamula amebainisha hayo alipokuwa akifungua Mkutano wa Pili (2) wa Uratibu wa Watendaji Wakuu wa Jumuiya za Kiuchumi za Kikanda (RECs) kuhusu utekelezaji wa Eneo Huru la Biashara la Afrika uliofanyika tarehe 7 Juni 2022 jijini Arusha.

Mkutano huo uliohudhuriwa na Wakuu wa Jumuiya za Kuichumi za Kikanda ulilenga kuwakutanisha Wakuu hao na Sekretariati ya AfCFTA ili kwa pamoja waweze kujadili na kuweka mikakati endelevu ya utekelezaji wa makubaliano ya AfCFTA. Mikakati hiyo ni pamoja na kubuni namna ya kupata rasilimali zitakazoiwezesha Sekretariati ya AfCFTA kuendesha shughuli zake bila kutegemea ufadhili wa nchi za nje, na kuandaa mfumo wa pamoja wa ushirikiano utakaoziwezesha pande zote mbili kutekeleza makubaliano ya AfCFTA kwa ufanisi.

Akizungumza kwenye ufunguzi wa Mkutano huo Waziri Mulamula alieleza kuwa uchumi wa Afrika utaendelea kukua kwa kasi zaidi endapo nchi za Afrika zifanikiwa kuunganisha shughuli za kiuchumi ikiwemo kuendesha biashara baina yetu wenyewe. Waziri Mulamula aliongeza kusema, anamatarajio makubwa kuwa ndoto za waasisi wa Umoja wa Afrika za kuwa na Afrika yenye umoja na iliyounganishwa kiuchumi zinaenda kutimia siku za usoni.

“Nina imani kubwa kuwa uwepo wa mikutano ya mfumo huu unaounganisha Sekretariati ya Eneo Huru la Afrika na Watendaji wa Jumuiya za Uchumi za Kikanda, utawezesha kupatikana kwa mapendekezo ya sera zinazotekelezeka na kujenga ushirikiano thabibiti ambao utawezesha kutatua changamoto mbalimbali zinazokwamisha ustawi wa biashara miongoni mwa nchi za Afrika, na hatimaye kufikia ndoto za waasisi wetu za kuwa na Afrika iliyounganishwa kiuchumi”. Alisema Balozi Mulamula

Vilevile Waziri Mulamula alieleza kuwa pamoja na jitihada za kuendelea kushirikiana katika kutekeleza makubaliano ya AfCFTA ni muhimu pia kwa Jumiya za Kiuchumi za Kikanda na Serikali za Afrika kuendelea kuwekeza katika ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji inayounganisha bara la Afrika ambayo itasadia kwa kiasi kikubwa kuokoa gharama na muda wa usafirishaji wa bidhaa na huduma miongoni mwa Nchi za Afrika.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Sekretarieti ya AfCFTA, Mhe. Wamkele Mene alisema kuwa utekelezaji wa Mkataba wa AfCFTA ni wa lazima kwa maendeleo ya Afrika hivyo ni muhimu pia kwa sekta binafsi kupewa kipaumbele kwenye utekelezaji wa makubaliano ya AfCFTA.

Mhe. Wamkele aliendelea kusisitiza kuwa ni muhimu kwa nchi za Afrika kuendelea kuhimiza katika ukuzaji wa viwanda na kuwekeza katika kuboresha bidhaa zake, ili kumudu ushindani wa soko la kimataifa na hatimaye kuweza kunufaika na soko kubwa katika biashara ya kimataifa na kuongeza mchango wake katika pato la Dunia. .

“Inasikitisha kuona kwamba nchi 55 za Afrika kwa sasa zinachangia asilimia 2 tu ya pato la biashara ya duniani na asilimia 3 ya Pato la Dunia huku Singapore, jiji lenye ukubwa wa maili 600 za mraba pekee, likichangia asilimia 6.2 ya biashara ya kimataifa”. Alisema Katibu Mkuu wa Sekretarieti ya AfCFTA Mhe. Wamkele.

Aidha, Mhe. Wamkele alisisitiza umuhimu wa ushirikiano thabiti na utendaji wa karibu kati ya RECs na Sekretarieti ya AfCFTA ili kuhakikisha kuwa matokeo ya AfCFTA yanawiana na maendeleo ya kikanda katika ushirikiano na ukuajia wa biashara.

Mkutano huu umefanyika ikiwa ni utelekezaji wa agizo la Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali ambalo uliielekeza Sekretariati ya AfCFTA, Tume ya Umoja wa Afrika na RECs kukaa pamoja na kuandaa mfumo wa ushirikiano sambamba na kuoanisha programu na shughuli zao ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa makubaliano ya AfCFTA

About the author

mzalendoeditor