Featured Kitaifa

MHANDISI KEMIKIMBA AZINDUA UTEKELEZAJI WA MRADI WA UJENZI LA BWAWA LA FARKWA

Written by mzalendoeditor

Naibu Katibu Mkuu, Mhandisi Nadhifa Kemikimba akiongoza kikao cha uzinduzi wa mradi wa ujenzi wa bwawa la Farkwa, jijini Dodoma.

Naibu Katibu Mkuu, Mhandisi Nadhifa Kemikimba akizungumza katika uzinduzi wa mradi wa ujenzi wa bwawa la Farkwa, jijini Dodoma.

Mhandisi Mkuu wa Rasilimali za Maji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, Benson Nkhoma akizungumza katika kikao cha uzinduzi wa mradi wa ujenzi wa bwawa la Farkwa, jijini Dodoma.

Wajumbe washiriki katika kikao cha uzinduzi wa utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa bwawa la Farkwa, jijini Dodoma.

Mkurugenzi wa Rasilimali za Maji Wizara ya Maji, Dkt. George Lugomela akiwasilisha mada katika kikao cha uzinduzi wa utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa bwawa la Farkwa, jijini Dodoma.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Nadhifa Kemikimba akiwa kwenye picha ya pamoja na wajumbe mara baada ya kuzindua utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa bwawa la Farkwa, jijini Dodoma.

……………………………….

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Nadhifa Kemikimba amezindua Awamu ya Kwanza ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa bwawa la Farkwa wenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 292 ambazo ni  mkopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), jijini Dodoma.

Mhandisi Kemikimba amesema lengo kuu la mradi huo ni kuimarisha upatikanaji wa huduma ya majisafi, salama na ya kutosha katika Jiji la Dodoma na Miji ya Bahi, Chemba na Chamwino. Vilevile, Mradi huo unatarajiwa kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii kutokana na mchango wa huduma ya maji katika maendeleo ya sekta za viwanda, kilimo, nishati, ujenzi na uchukuzi.  

Amesema kuwa hatua ya Serikali kuhamia Dodoma imeongeza kwa kiasi kikubwa imechangia kuongeza  mahitaji ya huduma ya maji na usafi wa mazingira, hivyo hatua mbalimbali zinachukuliwa na Serikali kuhakikisha  huduma ya maji inaimarika ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Bwawa la Farkwa.

Vilevile, Naibu Katibu Mkuu Mhandisi Kemikimba ameishukuru Benki ya Maendeleo ya Afrika kwa mchango wao katika maendeleo ya nchi kupitia ufadhili wa miradi ya maendeleo katika sekta za maji, elimu, nishati, ujenzi na uchukuzi. Miradi hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa kuifanya Tanzania kuwa kivutio kwa wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi.

Aidha, Mhandisi Kemikimba amewapongeza viongozi na watumishi wote wa Wizara ya Maji kwa kufanikisha maandalizi ya mradi huo pamoja na kusisitiza kuwa wizara itasimamia utekelezaji wa mradi huo kikamilifu ili kufikia malengo yaliyowekwa pamoja na kuhakikisha ufanisi katika matumizi ya fedha zilizopatikana. 

Akizungumza katika kikao hicho, Mhandisi  Mkuu wa Rasilimali za Maji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, Benson Nkhoma amesema utekelezaji wa awamu ya kwanza ya mradi utahusisha ujenzi wa bwawa la Farkwa; mtambo  wa kutibu maji; usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji; usanifu wa miundombinu ya kupeleka maji kutoka kwenye bwawa kwenda Jiji la Dodoma na miji ya Bahi, Chemba na Chamwino; usanifu wa miundombinu ya majitaka katika miji ya Bahi, Chemba na Chamwino; pamoja na kujenga uwezo katika usimamizi wa rasilimali za maji.

Mhandisi Nkhoma amesema kwa sasa Jiji la Dodoma linakadiriwa kuwa na idadi ya wakazi  500,000 na inatarajiwa kuongezeka kufikia 1,972,968 ifikapo  mwaka 2051. Aidha, hali ya upatikanaji wa huduma ya maji kwa mji wa Bahi ni asilimia 28; Chemba asilimia 50 na Chamwino asilimia 85 wakati upatikanaji wa huduma ya uondoaji wa majitaka katika miji hiyo ni asilimia 20. Hivyo, utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa mradi huo unatarajiwa kuimarisha huduma za majisafi na uondoaji wa majitaka katika miji hiyo. 

Mradi unatarajiwa kuetekelezwa kwa awamu mbili na kunufaisha wakazi wapatao milioni 2.5 kwa upande wa huduma ya majisafi na salama na wakazi milioni 1.5 wanatarajiwa kunufaika na huduma ya uondoaji majitaka. Matokeo ya muda mrefu ya mradi huo ni pamoja na kuimarika kwa afya kwa jamii, mazingira ya biashara na maendeleo ya jamii kwa ujumla.

About the author

mzalendoeditor