Featured Kitaifa

NEMC:’MAENEO YA STAREHE,NYUMBA ZA IBADA ZINAONGOZA KWA KELELE’

Written by mzalendoeditor
MENEJA wa Uzingatiaji wa Sheria na Ufuatiliaji kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi ya Mazingira (NEMC),Ndimbumi Mboneke,akizungumza wakati wa  warsha ya Maofisa Mazingira wa Mikoa na Wilaya jijini Dodoma.
………………………
Na Mwandishi Wetu_DODOMA
MENEJA wa Uzingatiaji wa Sheria na Ufuatiliaji kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi ya Mazingira (NEMC),Ndimbumi Mboneke,ameeleza kuwa nyumba za ibada na maeneo ya starehe yanaoongoza kwa kulalamikiwa kuwa kinara wa kelele.
Hayo ameyasema wakati wa  warsha ya Maofisa Mazingira wa Mikoa na Wilaya jijini Dodoma.
Mboneke amesema kuwa siku za hivi karibuni kumekuwapo na kero kubwa ya kelele, kutoka kwenye maeneo mbalimbali.
“Tumekuwa tukipokea malalamiko mengi sana tukiyachambua hayo malalamiko ya kelele mengi ni kutoka kwenye baa na nyumba za ibada, kiasi ni kutoka kwenye viwanda hasa vile vinavyotumia teknolojia ambazo sio nzuri,”ameeleza
Amefafanua Kuwa  kelele zina athari kubwa kwenye afya ya binadamu na mazingira.
“Watu washindwe kulala na akishindwa kulala anashindwa kufanya kazi zake za siku kwasababu anakuwa hajapata usingizi vizuri, Wanafunzi wanashindwa kusoma, wazee wanaathirika ambao ni wagonjwa na wanapata athari za kiafya,”amesema
Hata hivyo amesema kuwa kuna kanuni za usimamizi wa mazingira, kelele na mitetemo ya Mwaka 2015 ambazo zimeweka viwango vya juu vinavyoruhusiwa kuzalisha kelele.
“Hivyo viwango vimetofautina kwa muda, lakini pia kuna maeneo kama ya shule, chuo na maeneo tofauti, maeneo ya kazi, maeneo ya biashara,”amesema
Alitolea mfano viwango vya sauti vya juu katika shule na vyuo ni decibel(kizio cha kupima kiwango cha sauti) 45 kwa mchana na 35 kwa usiku huku kwenye makazi ni 50 kwa mchana na 35 kwa usiku.
Aidha amesema kuwa kutokana na tatizo hilo upo mwongozo wa kusimamia kelele na mitetemo ambao ulizinduliwa Septemba 2021, kila taasisi iliyopo kwenye mwongozo imepewa majukumu yake ya kusimamia masuala hayo ambapo msimamizi Mkuu ni Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira.
Hata hivyo Mboneke ametoa A wito kwa kila mdau anayehusika kusimamia mwongozo huo awajibike kwa majukumu yake yaliyoainishwa.

About the author

mzalendoeditor