Featured Kitaifa

NIKONEKT APP YAWA MKOMBOZI KWA WATANZANIA

Written by mzalendoeditor

Na Bolgas Odilo, Dodoma.
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Dodoma wamezidi kuwaweka karibu wateja wao kwa kupitia NIKONEKT APP.
NIKONEKT APP ni mfumo mpya wa kupata huduma za umeme popote ulipo nchini Tanzania kwa kupitia simu yako ya kiganjani au kompyuta.
Mfumo huo kwa Dodoma ulianzishwa tarehe 30 Mei 2022 na kuleta mapinduzi makubwa kwa Mkoa wa Dodoma.
Hayo yamebainishwa mapema leo na Afisa Uhusiano wa TANESCO Mkoa wa Dodoma Sarah Libogoma.
“Wiki hii tumezindua huduma hii ya NIKONEKT kwa hapa Dodoma na unatumika katika wilaya zote.
“Tumeshapata maombi mengi na mpaka kufikia leo Ijumaa Juni 3, 2022 tumeshawaunganishia umeme zaidi ya wateja 30 na hii ni ndani ya wiki moja tu.
” Na malengo yetu ni kuwaunganishia umeme zaidi ya wateja 6000 ndani ya miezi mitatu ijayo,” alisema Libogoma.
Aidha Libogoma alisema kuwa, lengo la mfumo huo ni kuhakikisha wateja wanapata huduma ya umeme popote walipo kwa urahisi.
“Mfumo huu wa NIKONEKT utarahisisha zaidi upatikanaji wa huduma kwa wananchi wote kwa sababu ni salama na rahisi.
Aliongeza, “ Unaweza kupata huduma za NiKONEKT kupitia tovuti yetu www.nikonekt.tanesco.co.tz au kama mwananchi ana simu janja apakue NIKONEKT APP ili aweze kupata huduma zetu kwa haraka zaidi kupitia simu yake ya mkononi.
“Kwa wenye simu za kawaida wanaweza kupiga *152*00# na utachagua Nishati kisha TANESCO hapo utaweza kupata huduma zetu,” alielekeza Libogoma.
Naye Charles Magawa, mkazi wa Miganga Dodoma mmoja kati ya watumiaji wa huduma hiyo ya NIKONEKT APP alikuwa na haya yakusema.
“Niliomba umeme kwa kutumia NIKONEKT APP na siku hiyo hiyo nikaunganishiwa umeme, sikuamini kwa sababu sio kawaida.
“Nawashauri na wenzangu watumie mfumo huu kwasababu hauna usumbufu wowote na ni rahisi sana kutumika.
“Unachotakiwa kuwa nacho ni kitambulisho chako cha NIDA (kitambulisho cha Taifa) ili uweze kuunganishwa na mfumo huu,” alisema Magawa.
Kwa upande wake Kalangu Shabani mkazi wa Chang’ombe mtumiaji wa mfumo huo alisema kuwa, anaunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kurahisisha maisha kwa wananchi
Pia aliwataka Watanzania watumie mfumo huo kwakuwa ni salama na unahudumiwa kwa haraka zaidi

About the author

mzalendoeditor