Featured Kitaifa

DCEA YATEKETEZA ZAIDI YA HEKARI 21 ZA BANGI MKOANI ARUSHA 

Written by mzalendoeditor
Kamishna Jenerali wa mamlaka ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya nchini (DCEA) Jenerali Jerald Kusaya akiongea na waandishi wa habari mkoani Arusha.
……………………………………………
NA NAMNYAK KIVUYO, ARUSHA 

Mamlaka ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya nchini (DCEA) imeteketeza hekari zaidi ya 21 ya mashamba ya dawa ya kulevya aina ya Bangi mkoani Arusha.

Akiongea na waandishi wa habari kamishna Jenerali wa mamlaka hiyo Jerald Kusaya alisema kuwa kuanzia Mei 20 hadi 23,2022 mamlaka hiyo kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na  usalama mkoani Arusha ilifanya oparesheni katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo na kufanikiwa kutekeleza mashamba hayo.
Alisema katika operesheni hiyo takriban kilo 220 za bangi zilikamatwa katika eneo la Usariver wilaya ya  Arumeru na Wilaya ya Monduli ambapo katika tukio hilo watu wanne wanashikiliwa kwa tuhuma za kuzalisha na kusafirisha dawa za kulevya aina ya Bangi.
“Hii oparesheni ni endelevu katika maeneo yote nchini, tunasaka aina zote za dawa za kulevya na tunaangalia ni namna gani tunaweza kukabiliana na hii biashara haramu,vtumeanza Arusha lakini tunaenda na maeneo mengine kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama,” Alisema Jenerali Kusaya.
“Tunaimani ya kwamba kama ilivyo katika mkoa wa Arusha bado Kuna maeneo ambayo yana mashamba  lakini na wananchi ambao wamehifadhi magunia mbalimbali ya Bangi hivyo zaidi tuwaambie wananchi kuwa hii ni vita kwamaana ya kwamba tunapambana na watu ambao wamekusudia zaidi kucheza na akili zetu,”
Hata hivyo ametoa rai kwa wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kwa kutoa taarifa za watu wanajihusisha na uzalishaji na usambazaji wa dawa ya kulevya ili kufikia Tanzania yenye kizazi kisichotumia Wala kujihisisha na biashara ya dawa za kulevya.

About the author

mzalendoeditor