Featured Kitaifa

SERIKALI KUJENGA HOSPITALI YA WILAYA, MWANGA MKOANI KILIMANJARO

Written by mzalendoeditor

Mkuu wa Wilaya ya Mwanga Abdalah Mwaipaya, Mbunge wa Jimbo la Mwanga Joseph Tadayo na Baadhi ya wananchi waliojitokeza katika UZINDUZI wa ujenzi wa Hospital ya wilaya ya Mwanga, Kilimanjaro

Mbunge wa Jimbo la Mwanga Joseph Tadayo akiteta jambo na Mchungaji Abraham Mshana wa KKKT Dayosisi ya Mwanga Mkoani Kilimanjaro Usharika wa Kwamsembea Usangi

Mbunge wa Jimbo la Mwanga Joseph Anania Tadayo akizungumza na vyombo vya habari

Mkuu wa Wilaya ya Mwanga Abdalah Mwaipaya,akizungumza na waandishi wa habari

………………………………………….

Na.Janeth Raphael-MWANGA
Baadhi ya wakazi wa Jimbo la Wilaya ya Mwanga Mkoani kilimanjaro wamejitokeza kushiriki zoezi la msaragambo kusafisha na kuchimba msingi kwa ajili ya maandalizi ya ujenzi wa hospitali ya mpya ya kisasa Wilayani hapo

Ujenzi huo wa hospitali ya Wilaya unatarajiwa kuanza na kwamba tayari Serikali imeshatoa fedha za awamu ya kwanza shilingi bilion 1 ambapo gharama yote ya ujenzi mpaka kukamilika inakadiriwa kuwa shilingi za Kitanzanja bilioni 3.

Akizungumza mara baada ya zoezi hilo Mbunge wa jimbo la Mwanga Joseph Tadayo amesema kuwa ujenzi wa hospitali hiyo ni moja ya ahadi ya mheshimiwa Rais wakati wa kampeni ya uchaguzi mkuu mwaka 2020 kutokana na Wananchi wa ukanda wa tambarare wanaokabiliwa na changamoto za huduma ya afya na kufuata hospitali ya Wilaya usangi na hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro mawenzi.

Mbunge Tadayo amesema kukamilika kwa hospitali hiyo kutapunguza adha kwa
wananchi kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya mbalimbali katika hospitali ya Wilaya usangi ambayo iko mlimani na kwamba wananchi wa ukanda wa tambarare wanashindwa kufika kwa urahisi.

Tadayo ameendelea kusema kuwa kukamilika hospitali hiyo kutaboresha upatikanaji wa huduma za afya ndani ya Mwanga na wilaya jirani za Same na Moshi vijijini hata kwa wasafiri kutokana na hospitali hiyo kujengwa jirani na barabara kuu iendayo Dar es salaam-Arusha.

“Hospitali hii ni yakisasa pia iko barabara kuu iendayo Dar es salaam -Arusha hivyo ni rahisi inapotokea ajali za barabarani (hatuombei hivyo) majeruhi watapatiwa huduma kwa haraka badala ya kupelekea hospitali ya rufaa mawenzi au hata hospitali ya Kanda KCMC ambapo pia ni mbali,” – amesema.

Amesema mpango huu wa ujenzi wa hospitali ya Wilaya katika ukanda huu wa tambarare ni mpango wa muda mrefu wa wazee wa Mwanga na baba wa Mwanga Mzee David Cleopa Msuya ambapo walikaa nakutenga eneo zaidi ya ekari 53.

“Kwa zaidi ya miaka 30 wananchi wamekuwa wakisubiri ujenzi wa hospitali hiyo ambapo Serikali ya awamu ya sita imetoa fedha kwa ajili ya
kukamilisha ujenzi huo,”amesema.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mwanga Abdallah Mwaipaya amesema Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu imetoa fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi na kuwataka wananchi wa Mwanga kutoa ushirikiano ili kukamilisha ujenzi huo kwa wakati.

“Shilingi bilion moja za awamu ya kwanza kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya wilaya zimeshaletwa na tayari eneo lilikwisha tengwa kwa muda mrefu na linahati miliki na mali ya halmashauri hivyo na mwahidi Mheshimiwa Rais Samia Suluhu kwamba tutasimamia vema ujenzi huo ,”amesema Mwaipaya.

About the author

mzalendoeditor