Featured Kitaifa

MAGEUZI MAKUBWA SEKTA YA ELIMU 2024/25

Written by mzalendoeditor

 

Waziri WA Elimu,Sayansi na Teknolojia Prof.Adolf Mkenda,akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2024/25 Leo Mei 7,2024 jijini Dodoma.

Na.Alex Sonna_DODOMA

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda amepanga kutumia Sh.Trilioni 1.96 kwa mwaka 2024/25 ili kutekeleza vipaumbele vitano vyenye lengo la kuongeza ubora wa elimu kwa kuwezesha vijana wa Kitanzania kupata maarifa, ujuzi, kujiamini, kujiajiri na kuajirika.

Vilevile, vipaumbele vyenye kujielekeza katika kutegemeza tafiti, sayansi, teknolojia na ubunifu katika agenda ya maendeleo ya nchi.

Akiwasilisha bungeni jana makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2024/25, Prof. Mkenda alisema serikali itaendelea na utekelezaji wa sera na mitaala, mapitio ya sheria na kuandaa miongozo ya utoaji elimu na mafunzo nchini.

Alisema kipaumbele kingine ni kuongeza fursa na kuimarisha ubora wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi (amali na amali sanifu);Kuongeza fursa na kuimarisha ubora wa elimu ya msingi, sekondari na ualimu;kuongeza fursa na kuimarisha ubora wa elimu ya juu na kuendeleza tafiti, matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu.

MAGEUZI KWENYE MITAALA

Alisema serikali itafanya mapitio ya mitaala 171, kuandaa mitaala mipya 18, kuanzisha programu za vipaumbele 145 pamoja na matumizi ya mbinu bunifu za ufundishaji katika elimu ya juu. Aidha, itawezesha ziara za kimkakati kwa wafanyakazi wa sekta ya elimu katika nchi zenye uzoefu wa uandaaji wa rasilimaliwatu yenye maarifa na ujuzi wenye kuchangia katika ukuaji wa kati wa uchumi.

Pia, alisema itaanzisha vituo vya elimu huria ili kuimarisha majukwaa ya ndani na kuongeza fursa za upatikanaji wa elimu ya juu; itasasisha na kuandaa mtaala mpya katika taasisi 17 za elimu ya juu; na kuhakiki mitaala 230 ya vyuo vya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi.

“Lengo ni kuhakikisha kuwa mafunzo yanayotolewa yanakidhi mipango ya nchi, soko la ajira la kitaifa na kimataifa na kuwawezesha wahitimu kujiajiri na kukabiliana na tatizo la ukosefu wa ajira,”alisema.

Kadhalika, alisema itaandaa mwongozo wa elimu jumuishi wa ufundishaji na matumizi ya teknolojia kwa lengo la kuongeza ufanisi katika ufundishaji na matumizi ya teknolojia katika elimu na mafunzo.

Pia alisema itafanya mapitio ya mwongozo wa uanzishaji na usajili wa shule wa mwaka 2020 ili kuendana na mabadiliko ya sera na mitaala;itakamilisha mwongozo wa kuwatambua na kuwaendeleza wanafunzi wenye vipawa na vipaji.Kuongeza Fursa na Kuimarisha Ubora wa Mafunzo ya Amali (Ufundi na Ufundi Stadi) katika Shule za Sekondari na Vyuo vya Amali

SHULE 100 ZA AMALI KUJENGWA

Katika kuhakikisha tunaongeza fursa za amali nchini, alisema serikali itaendelea kuboresha na kuongeza miundombinu ya shule za

sekondari za amali, vyuo vya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi.

Alisema serikali itawezesha ujenzi wa shule mpya 100 za sekondari za ufundi, kati ya hizo shule 26 zitaanza kupokea wanafunzi kuanzia Januari 2025.

Aidha, ujenzi wa shule za amali utapewa kipaumbele katika maeneo ambayo hayana vyuo vya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi au shule ya amali ya sekondari.

Alisema pia itaendelea na ujenzi wa karakana nne kwa ajili ya fani ya umeme, ufundi bomba, ufundi magari na ujenzi katika Chuo cha Ufundi na Mafunzo Stadi – Kihonda pamoja na ujenzi wa karakana ya ufundi bomba katika Chuo cha Ufundi na Mafunzo Stadi cha Mkoa wa Mbeya.

“Seriakli itadahili wanafunzi 263,718 wa elimu ya ufundi na mafunzo na ufundi stadi ambapo wanafunzi wa vyuo vya elimu ya ufundi ni 190,518 na wanafunzi wa vyuo vya mafunzo ya ufundi stadi ni 73,200 sawa na ongezeko la asilimia 23 ikilinganishwa na udahili wa mwaka 2023/24. Udahili unalenga kuongeza rasilimaliwatu yenye ujuzi na uwezo wa kujiajiri na kuajiriwa,”alisema.

Pia alisema itatoa mafunzo ya muda mrefu na muda mfupi kwa watumishi 215 ambapo mafunzo ya muda mrefu ni watumishi 50 na muda mfupi ni 165 kwa watumishi wa vyuo vya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi na shule za sekondari za elimu ya amali kuhusu mipango ya elimu na ufundishaji unaozingatia ujenzi wa umahiri.

“Itatoa mafunzo kwa walimu 1,000 wa vyuo vya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi kuhusu tathmini ya mitaala ya umahiri (CBET) ili kuwawezesha walimu kufundisha na kufanya tathmini ya wanafunzi kwa kuzingatia umahiri,”alisema.

Kadhalika, alisema katika kugharimia elimu ya amali serikali itawezesha mafunzo kwa vitendo viwandani kwa wanafunzi 1,724 (Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya 551, Chuo cha Ufundi Arusha 500 na Taasisi ya Tekonolojia Dar es Salaam 673).

Vilevile, itaendelea kuwezesha upatikanaji wa chakula kwa wanafunzi 17,411 (vyuo vya maendeleo ya wananchi wanafunzi

15,000, Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam wanafunzi 850, Chuo cha Ufundi Arusha wanafunzi 800 na Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya wanafunzi 761).

MIKOPO KWA WANAFUNZI

Aidha, alisema serikali itatoa mikopo kwa wanafunzi wa stashahada takribani 10,000 katika fani za kipaumbele na zenye uhaba wa wataalam nchini ikiwamo fani za sayansi na ufundi.

Aidha, alisema ili kuwezesha na kuimarisha huduma ya utoaji na upatikanaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu wenye sifa na uhitaji, Serikali itatekeleza itaongeza fursa za mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu kutoka 223,201 hadi 252,245.

“Itatoa mikopo kwa wanafunzi 84,500 wa mwaka wa kwanza ambapo shahada ya kwanza 80,000, shahada za juu 2,000, wanaosoma nje ya nchi 500 na Samia Scholarship 2,000,”alisema.

Pia alisema itatoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi 40 wenye ufaulu wa juu kwenye masomo ya Sayansi hususan wanafunzi wa kike waliohitimu Mtihani wa Taifa ya Kidato cha Sita na shahada ya awali kupitia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Alisema itaendelea kukusanya madeni ya mikopo iliyoiva ya kiasi cha Sh. Bilioni 198 kutoka sekta ya umma na kuimarisha makusanyo kutoka sekta binafsi na isiyo rasmi.

Aidha, itatafuta wanufaika wapya 40,000 wenye marejesho ya mikopo iliyoiva ikijumuisha wanufaika wapya 5,000 wenye mikopo chechefu kutoka sekta binafsi na isiyo rasmi.

Pamoja na hayo itaanza kutoa ufadhili kwa ajili ya shahada za juu ikiwemo eneo la fani ya mionzi na nyuklia.

UPATIKANAJI VITABU

Alisema serikali kwa kipindi hicho itachapa na kusambaza nakala za vitabu takribani 2,000,000 vya masomo ya hisabati na sayansi kwa kidato cha 1 hadi 4.

Katika kuhakikisha wanafunzi wa sekondari na vyuo vya ualimu wanajifunza kwa vitendo, alisema serikali itanunua vifaa vya maabara kwa ajili ya shule 1,322 na vyuo 13 vya ualimu pamoja na vifaa vya kufundishia na kujifunzia katika vyuo 35 vya ualimu.

Vilevile, itanunua vifaa vya kujifunzia na kemikali kwa ajili ya kufundishia masomo ya sayansi kwa wanafunzi wa elimu kwa njia mbadala kwa hatua ya I na II.

Alisema katika kutoa fursa kwa wanafunzi walioacha shule kwa sababu mbalimbali, Serikali itaongeza fursa za utoaji wa elimu ya sekondari kwa njia mbadala kwa kuongeza udahili wa wanafunzi kutoka 22,131 kwa mwaka 2023/24 hadi 24,891 kwa mwaka 2024/25.

Vilevile, alisema itaongeza udahili wa wanafunzi wa astashahada, stashahada na shahada kutoka 4,430 hadi 5,300.

Hata hivyo, alisema itaunda mabaraza ya tasnia katika vyuo vikuu ambayo yatahusisha wataIaam, wajasiriamaIi na wabobezi katika aina mbaIimbaIi za ujuzi, maarifa na stadi zinazohitajika katika soko Ia ajira.

ViIeviIe, mabaraza yatashiriki katika kuhakikisha miundombinu inayoaandaIiwa inakuwa rafiki kwa watumiaji wote wakiwemo wenye mahitaji maalum.

About the author

mzalendoeditor