Featured Kitaifa

SIDO WAKUTANA NA WADAU KUJADILI SEKTA NDOGO YA MAFUTA YA ALIZETI.

Written by mzalendoeditor

Meneja wa Masoko Shirika la Kudumia Viwanda Vidogo Tanzania (SIDO), Bi. Lilian Massawe akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kuhusu sekta ndogo ya mafuta ya alizeti, ambapo wadau mbalimbali wamekutana kwa ajili ya kujadili na kuweka mipango mikakati endelevu ya namna gani wanaweza kuboresha zao hilo la alizeti.

Meneja wa SIDO Mkoa wa Dodoma Bw. Stempeho Nyari akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kuhusu mipango mikakati endelevu ya namna gani wanaweza kuboresha zao la alizeti kupitia viwanda vidogo hapa nchini.

Mwenyekiti wa Chama cha Wazalishaji wa Mafuta ya Alizeti Tanzania (TASUPA) Bw. Ringo Iringo akitoa ufafanuzi kuhusu uzalishaji wa mafuta wa alizeti.

Wadau wa sekta ndogo ya Mafuta ya Alizeti wakiwa katika kongamano jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kujadili na kuweka mipango mikakati endelevu ya namna gani wanaweza kuboresha zao la alizeti ili liweze kusaidia Taifa na kupiga hatua katika nyanja mbalimbali za kiuchumi.

…………………………………

NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM.

Shirika la Kudumia Viwanda Vidogo Tanzania (SIDO) wamekutana na wadau wa sekta ndogo ya Mafuta ya Alizeti kwa ajili ya kujadili na kuweka mipango mikakati endelevu ya namna gani wanaweza kuboresha zao la alizeti ili liweze kusaidia Taifa kwa kuweka malengo ya muda mfupi na mrefu. 

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Meneja wa SIDO Mkoa wa Dodoma Bw. Stempeho Nyari, amesema kuwa mafuta ya alizeti yameonekana kuwa uhitaji mkubwa hapa nchini licha ya kuwepo na juhudi zinazofanywa na sekta binafsi katika kuzalishaji. 

Bw. Nyari amesema kuwa SIDO imekuwa ikitoa huduma ya kuwasaidia viwanda vidogo katika Mikoa yote inayozalisha zao la alizeti ikiwemo Mkoa wa Dodoma, Singida pamoja na Manyara ili kuhakikisha kunakuwa na mazingira rafiki.

“Tumekuwa tukitoa mafunzo kwa watu wetu na kuwapatia Teknolojia ili waweze kuzalisha mafuta yenye ubora yaliothibitisha na Shirika la Viwango Tanzania (TBS)” amesema Bw. Nyari.

Amefafanua kuwa mpaka sasa kuna wakulima zaidi ya milioni moja wanaolima zao la alizeti, lakini uzalishaji bado ni mdogo ukilinganisha na uhitaji kwa watumiaji.

Bw. Nyari ameeleza kuwa kwenye kilimo cha alizeti kuna fursa kubwa ya kiuchumi, hivyo amewataka watanzania kuchangamkia fursa hiyo ili waweze kupiga hatua katika nyanja mbalimbali za kimaendeleo.

“Tunaendelea kuwashawishi wazalishaji waongeze ubora wa mafuta ya alizeti, kwani sekta ndogo ya mafuta ya alizeti ina umuhimu kwa taifa, wananchi wanaweza kujiajiri kuanzia shambani, viwandani na kufanikiwa kupunguza umaskini kwa kiwango kikubwa” amesema Bw. Nyari.

Amebainisha kulingana na ukubwa wa soko bado kuna uhitaji wa wakulima zaidi ya milioni mbili ili waweze kuzalisha mbegu za alizeti jambo ambalo litasaidia kuongeza mchango mkubwa katika kuchakata mafuta ya alizeti.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji Shirika la Kudumia Viwanda Vidogo Tanzania (SIDO), Meneja wa Masoko wa SIDO Bi. Lilian Massawe, amesema kuwa uhitaji wa mafuta ya alizeti hapa nchini Tanzania ni tani 650, lakini uwezo wa kuzalisha ni tani 250 hadi 300.

Bi. Massawe amesema kuwa asilimia 70 ya uhitaji inatokana  na zao la alizeti, hivyo SIDO inaendelea kuwahamasisha wakulima na walizalishaji ili kuongeza wigo.

“Watanzania wanatakiwa kuja SIDO kwa ajili ya kupata ushauri wa kuzalisha zao la alizeti pamoja kuanzisha viwanda vidogo” amesema Bi. Massawe.

Mwenyekiti wa Chama cha Wazalishaji wa Mafuta ya Alizeti Tanzania (TASUPA) Bw. Ringo Iringo, amesema kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye viwanda vingi vya kuzalisha mafuta ya kula Afrika ikiwa na uwezo wa kuzalisha tani 3,500 kwa siku.

Bw. Iringo ameeleza kuwa kuna changamoto kubwa ya upatikanaji wa mbegu za alizeti kutoka kwa wakulima, kwani kwa mwaka wanapata tani 1,130 na kusababisha viwanda vingi kufanya kazi chini ya uwezo wake.

Amesema kuwa maitaji ya upatikanaji wa mbegu za alizeti kwa mwaka tani 5, 100, lakini inayopatikana katika masoko ni tani 450 na kufanya tani 4,500 kukosekana katika soko na kufanya kusindwa kuzalisha mafuta ya alizeti.

”Tunatakiwa kufanya uwekezaji kwa kuwekeza katika mashamba makubwa kwa kutumia kilimo cha kisasa cha mafuta ya alizeti, pia tunaomba taasisi za fedha wabadilishe mifumo yao ya ukopeshaji kwa kuweka mikopo ya uwekezaji na sio mikopo ya biashara” amesema Bw. Iringo.   

Katika hatua nyengine ameipongeza serikali kwa jitaida mbalimbali wanazofanya katika kuhakikisha kunakuwa na mazingira marafiki ya uwekezaji.

About the author

mzalendoeditor