Featured Kitaifa

KIPANGA ARIDHISHWA NA UJENZI WA MAJENGO YA CHUO CHA VETA SAMUNGE

Written by mzalendoeditor

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Omari Kipanga  ameupongeza Uongozi wa Chuo Cha Ufundi Arusha kwa usimamizi mzuri wa ujenzi wa baadhi ya majengo ya Chuo Cha VETA Samunge unaoendelea hivi sasa wilayani Ngorongoro mkoani Arusha.

Waziri Kipanga ametoa pongezi hizo wakati alipofanya ziara kukagua miradi ya elimu inayotekelezwa mkoani humo ambapo amesema ameridhishwa na namna chuo hicho kinavyosimamia ujenzi wa majengo ya Chuo hicho.

“Hapa Samunge kazi ni nzuri nimeridhishwa sana na maendeleo ya ujenzi wa majengo mapya ya bwalo, bweni la wasichana na wavulana sambamba na nyumba za watumishi,” amesema Mhe Kipanga.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri Kipanga ameutaka Uongozi wa Wilaya ya Ngorongoro kuhakikisha unasimamia vizuri utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa chuo cha Ualimu Ngorongoro ili fedha zilizotengwa zaidi ya Bilioni 1.9 zitumike kama zilivyopangwa na thamani ya fedha iweze kuonekana.

“Mnatakiwa kusimamia mradi huu kwa weledi mkubwa na mtambue lengo la Chuo hiki, wengi wenu mnasimamia mradi huu bila kusoma michoro. Mhandisi pitia vyema michoro ya majengo haya yasije yakapishana na majengo mengine,” amesisitiza Mhe. Kipanga.

Aidha Naibu Waziri Kipanga amemuomba Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kushirikiana vyema na wasimamizi wa mradi wa Chuo cha Ualimu sambamba na Chuo Cha VETA Samunge ili ujenzi ukamilike kwa wakati.

Kwa Upande wake Mthibiti ubora wa Shule Wilaya ya Ngorongoro, Josephat Kirongwa amemuhakikishia Naibu Waziri kuwa atakwenda kusimamia vyema ujenzi wa Chuo hicho Ili kiweze kukamilika kwa wakati na thamani ya fedha ionekane.

About the author

mzalendoeditor