Featured Kitaifa

MBUNGE MTATURU ALILIA KITUO CHA POLISI IKUNGI

Written by mzalendoeditor

MBUNGE wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu ameomba mambo matatu kwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ikiwemo kituo cha Polisi katika wilaya ya Ikungi na kuahidi kushika Shilingi endapo hatopata jibu la kuridhisha kuhusu ombi hilo.

Mtaturu ametoa maombi hayo Mei 5,2022,Bungeni Jijini Dodoma wakati akichangia mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023.

Akichangia mjadala huo Mtaturu amesema kituo cha polisi kilichopo Ikungi kimeanza ujenzi katika miaka saba iliyopita.

“Ndani ya bunge hili nimeuliza maswali sio chini ya mara tatu kuulizia kituo kile na majibu yamekuwa ni yale yale,kwenye kituo cha polisi kinachotumika sasa hivi mnaweza kusema ni stoo, sio kituo cha polisi chenye hadhi ya jeshi la polisi ,

“Nimeona hapa imetajwa ndani ya bajeti na Mh Masauni tuliongea na wewe umeshafika pale 2018 ukiwa Naibu Waziri ,nikuombe sana kama sitopata majibu yakutosheleza kwa hakika kwa mara ya kwanza nitashika shilingi ili nipate ufafanuzi wa kutosha juu ya kituo cha Ikungi lakini na vituo vingine nchini, nini mkakati wa serikali katika kuhakikisha vituo hivyo vinajengwa na kuweka hadhi ya jeshi la polisi ambalo linafanya kazi vizuri sana,”alisisitiza.

Jambo la pili aliloliomba Mtaturu ni kuhusu vyombo vya usafiri ambapo kwa mujibu wa ukubwa wa eneo la Ikungi magari yaliyopo ni chakavu na hayakidhi mahitaji.

“Tumeambiwa hapa wilaya ya Ikungi ina Kilomita za mraba 5,800 ni wilaya kubwa lakini ina magari mawili ambayo ni chakavu sana,ukihitaji leo waende waka attend tukio lolote wanaweza wakaenda ,lakini kabla hawajarudi wanaambiwa tukio lingine limetokea,kwa hiyo hawawezi kuwahi matukio mbalimbali,”alisema.

Amesema yeye mbunge alishawahi kuwachangia pikipiki mbili ili kupunguza makali hayo na hivyo kumuomba Waziri awapatie gari katika mgao wa magari .

“Niombe angalau watuongezee gari lingine moja ili kumsaidia OCD aweze kufanya kazi vizuri yeye na watu wake,lakini pia kwenye hili ni OC ya mafuta,tunategemea nini tunapokuwa tunaamini tunawawekea ration ndogo sana ya mafuta kwa mwezi,

“Unategemea huyu OCD atafanyaje kazi kilomita 300 kwenda na kurudi kila siku kwa matukio ,itakuwa niajabu sana unaruhusu aka attend matukio wakati hujamuwezesha ,niombe waziri tuwaongezee bajeti ili polisi waweze kufanya kazi yao vizuri na kuweza kuokoa watanzania na mali zao,”alisisitiza.

Suala la tatu ambalo ameliomba ni kuhusu mafao ya polisi ambao wanafanya kazi nzuri na kwa uzalendo mkubwa.

“Na kama ulivyosikia mishahara yao ni midogo lakini inapofika amestaafu mafao yake hayapati kwa wakati,hii inashangaza sana mtu amefanya kazi zaidi ya miaka 30 lakini siku anastaafu unaenda kumuomba vielelezo vya kudai mafao yake, hili Mh Spika sio sawa,

“Niwaombe serikali iweze kuona namna ya kuwasaidia wazee wetu hawa waweze kuendelea kuishi vizuri na wengine wanapostaafu wanakufa haraka kwa sababu wanachelewa kulipwa mafao yao,”aliongeza.

PONGEZI KWA WAZIRI.

Mtaturu amempongeza Waziri wa wizara hiyo Mhandisi Hamad Masauni na wasaidizi wake kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuhakikisha usalama wa nchi kama walivyokasimiwa madaraka na Mh Rais Samia Suluhu Hassan.

“Wizara hii ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi yetu kama hakuna usalama hakuna maendeleo kwa hiyo haya tunayoshauri lengo letu ni kuhakikisha usalama wa Tanzania na kwa hakika waweze kufanya kazi yao vizuri,mfano mzuri panya road wameweza kuharibu sana amani ya wananchi katika maeneo ya Dar es salaam,”alisema.

PONGEZI KWA SPIKA.

Mtaturu amempongeza Spika Dkt Tulia Ackson kwa kuruhusu mjadala wa bei ya mafuta kuendelea bungeni na kusema alichofanya ni jambo kubwa katika Taifa.

“Leo asubuhi umefanya jambo kubwa katika Taifa la kuweza kuruhusu mjadala ambao una maslahi makubwa katika Taifa letu,tumepata salamu nyingi kutoka kwa watanzania kwamba bunge sasa linaenda kuishauri serikali na kwa muda muafaka na tunategemea maagizo yako yatatekelezwa,”alipongeza.

About the author

mzalendoeditor