Featured Kitaifa

ALIYEVUNJA VIOO VYA SHULE GAIRO ATUPWA JELA MIAKA MIWILI

Written by mzalendoeditor

NA FARIDA MANGUBE, MOROGORO.

Mtu moja aliyevunja vioo vya shule ya sekondari Kibedya iliyopo Wilaya ya Gairo Mkoani Morogoro amehukumiwa kifungo cha miaka miwili jela huku mlinzi wa shule hiyo akihukumiwa miezi sita kwa kosa la kuacha lindo lake na kusababisha uharibifu wa uvunjwaji wa vioo kumi na mbili katika shule hiyo.

Kuvunjwa kwa vioo kumi na mbili vya madarasa sita yaliojengwa kwa fedha za miradi ya Uviko 19 katika shule ya sekondari Kibedya Wilaya ya Gairo kumeisababishia hasara serikali ambapo kiasi cha shilingi milioni moja na laki tano zimetumika kukarabati madirisha ya madarasa hayo.

Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara na wananchi wa Kata ya Kibedya Mkuu wa Wilaya ya Gairo Bwana Jabiri Makame amesema hatua mbalimbali zimechukuliwa kwa waliofanya uharibifu huo ikiwemo kuhukumiwa kifungo cha miaka miwili jela kwa alivunja vioo hivyo huku mlinzi wa shule hiyo akihukumiwa miezi sita jela.

Aidha makame amesema serikali haitomfumbia macho mtu yeyote atakaye haribu mali za umma katika Wilaya hiyo huku akiitaka taasisi ya kuzuiya na kupambana na rushwa TAKUKURU Wilaya ya Gairo kufanya uchunguzi kwenye miradi ya ujenzi wa shule na kubaini kama kuna ubadhirifu wa wowote wa matumizi ya fedha.

Makame amefikia hatua hiyo ya kuigiza TAKUKURU baada ya kufanya ziara katika shule ya sekondari Kibedya ili kujionea maendeleo ya ujenzi wa vyumba vya madarasa,vyoo pamoja na maabara kwa ajili ya wanafunzi kujifunza kwa vitendo na kubaini uwepo wa ubadhirifu wa matumizi ya fedha za umma.

 “Niwaombe wananchi wa Kata ya Kibedya kuacha tabia kuharibu miundombinu ya miradi ya maendeleo sio kwenye shule tu hata kwenye miradi mingine kwani atakaye fanya uharibifu wowote atachukuliwa hatua za kisheria na niwambie tu serikali inamkono mrefu.” Alisema DC Makame.

“Nilifika hapa niliambiwa viti vipo kwa fundi na vitaletwa baada ya kukamilika lakini leo pia napewa taarifa tofauti na viti sivioni hivyo kwa sintofahamu hii naomba niiagize TAKUKURU kufanya uchukuzi hapa na Wilaya nzima ya Gairo juu ya matumizi ya fedha zilizoletwa na serikali kwaajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa.”Alisema

kwa upande wake diwani wa kata ya kibedya Bunditi Masatu amelaani kitendo kilichofanyika cha kuvunjaji wa vioo vya shule hiyo na kuwataka wananchi kuacha tabia ya kuharibu mali za sekali kwani atakaye bainika sheria itafuata mkondo wake.

About the author

mzalendoeditor