Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo April 11,2022 katika katika uwanja wa ndege jijini Dodoma kabla ya kuanza ziara ya kuzunguka nchi nzima kufanya uhamasishaji wa uwekaji anuani za makazi.

………………………………………………

Na Bolgas Odilo-DODOMA

WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye  ameanza ziara ya kukagua na kuhamasisha utekelezaji wa Operesheni ya Anwani za Makazi katika mikoa ya Tanga, Kilimanjaro na Arusha

Akizungumza na waandishi wa habari leo April 11,2022 jijini Dodoma kabla ya kuanza ziara hiyo ,Waziri Nape amesema tathmini inaonesha utekelezaji wa operesheni hiyo ni asilimia 69 huku baadhi ya maeneo yakiwa na changamoto na kutofanya vizuri.

Waziri Nape ameitaja mikoa ya Tanga na Dar es Salaam kuwa bado haijafanya vizuri kwenye uwekaji wa anuani za makazi.

“Kwa muda uliobaki tumekubaliana tuongeze nguvu kwa kutoka ofisini na kuifikia mikoa yote nchi nzima ili kukagua na kuhamasisha utekelezaji wa operesheni ya Mfumo wa Anwani za Makazi unaojumuisha ukusanyaji wa taarifa, kuweka taarifa kwenye mfumo wa kidijitali na uwekaji wa namba za nyumba, majina ya barabara na mitaa”,amesema Waziri Nape.

Aidha amesema kuwa Operesheni ya anwani za makazi inalenga kuhakikisha kila mtanzania anatambulika mahali alipo, mahali anapofanyia kazi/biashara na anapoishi hivyo ushirikiano wa pamoja utaifanya nchi ya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi ambazo unaweza kupata huduma ukiwa nyumbani kwako

“Katika mazingira haya ya dunia inayokwenda kidigitali si vema kwa nchi kuachwa nyuma, tumuunge mkono Mhe. Rais Samia kwenye operesheni hii na tujitendee haki watanzania kwa kuhakikisha tunakuwa na Anwani za Makazi”,ameeleza

Katika  ziara hiyo Waziri Nape ameambatana na Dkt. Jim Yonazi, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo pamoja na baadhi ya wataalamu ambapo wanatumia usafiri wa helkopta ili kuifikia mikoa zaidi ya mitatu kwa siku, kwa kuwa zoezi hilo ni operesheni maalumu na Wizara imejipanga kwenda kuona mwenendo wa utekelezaji na kuongeza nguvu maeneo yenye Changamoto.

Previous articleWATAALAMU WAZAWA WAZIBUA MISHIPA PACHA YA MOYO ILIYOZIBA KWA ASILIMIA 95
Next articleBARABARA YA SONGWE – VWAWA KUKAMILIKA JUNI, 2022

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here