Featured • Kitaifa

RC SENYAMULE AKAGUA MIRADI YA SH BILIONI 8.7 MPWAPWA

Written by Alex Sonna

Na Alex Sonna, DODOMA

MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Staki Senyamule, amekagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo yenye thamani ya Sh bilioni 8.7 katika Wilaya ya Mpwapwa, huku akisisitiza usimamizi madhubuti, uwajibikaji na kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati na ubora uliokusudiwa.

Miradi iliyokaguliwa inahusisha sekta za utawala, afya na elimu, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa, majengo ya Chuo cha Afya na Sayansi na Mazingira Shirikishi (MIHAS), nyumba za watumishi pamoja na ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Mzase.

Katika ziara hiyo , Senyamule amesema Serikali imetoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo, hivyo ni wajibu wa viongozi na watendaji wanaosimamia kuhakikisha zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na kuleta thamani halisi ya fedha.

Miongoni mwa miradi aliyokagua ni ujenzi wa jengo la Ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa, ambao hadi sasa umetumia Sh bilioni tatu na umefikia hatua za umaliziaji. Pia amekagua ujenzi wa uzio, nyumba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri na nyumba za Wakuu wa Idara wenye thamani ya Sh milioni 550 kutoka Serikali Kuu.

Aidha, amekagua ujenzi wa jengo la taaluma katika Chuo cha Afya na Sayansi na Mazingira Shirikishi (MIHAS), kilichopo Ilolo, unaogharimu Sh bilioni 4.65 kupitia ufadhili wa Benki ya Dunia na Wizara ya Afya. Jengo hilo litakapokamilika litakuwa na maabara sita, madarasa sita, ofisi na vyoo kwa ajili ya kuboresha mazingira ya mafunzo na kuongeza uwezo wa chuo kuzalisha wataalamu.

Katika sekta ya elimu, Mkuu huyo wa Mkoa amekagua ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari ya Mzase unaotekelezwa kupitia Mradi wa Kuboresha Elimu ya Sekondari (SEQUIP), kwa gharama ya Sh milioni 544.2, ukiwa na lengo la kuongeza fursa za elimu na kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji.

Mbali na ukaguzi wa miradi, Senyamule ametembelea shamba la Mwalimu Teresia Kimaro, linalozalisha matunda mbalimbali yakiwemo mapapai, mikomamanga, mitofaa, migomba na zabibu, ambapo amewahimiza wananchi kuiga mfano huo kwa kutumia ardhi waliyonayo kufanya kilimo cha kibiashara.

Amesema kilimo ni fursa muhimu ya kukuza kipato na kujenga uchumi wa familia, huku akiwataka wananchi kuchangamkia kilimo cha zao la tufaa ambalo limepewa kipaumbele katika Mkoa wa Dodoma.

Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Mzase, Kata ya Berege, katika mkutano wa hadhara, Senyamule amewahimiza kujiunga na mpango wa Bima ya Afya kwa Wote ili kujihakikishia upatikanaji wa huduma za matibabu na kujikinga na gharama za matibabu zinazoweza kuyumbisha uchumi wa familia.

Amesema ugonjwa unaweza kumpata mtu wakati wowote bila taarifa, hivyo kuwa na bima ya afya ni hatua muhimu katika kulinda afya na uchumi wa familia.

Katika mkutano huo, amesisitiza pia umuhimu wa kudumisha amani, upendo na uvumilivu katika jamii, akiwataka wananchi kutatua tofauti zao kwa kufuata sheria na taratibu zilizowekwa badala ya kujichukulia sheria mkononi.

Amekemea vitendo vya ukatili, mauaji na kujitoa uhai, huku akiwataka viongozi wa vijiji na kata kuimarisha utoaji wa elimu kwa wananchi na kusimamia sheria ili kuzuia matukio yanayohatarisha maisha.

Vilevile, amewataka wananchi kutumia kikamilifu msimu wa kilimo kwa kulima maeneo yote yanayofaa, kutunza mazingira, kuhifadhi misitu na kulinda miti ya asili ikiwemo mibuyu ambayo ni sehemu ya utambulisho wa Mkoa wa Dodoma.

Katika eneo la elimu, amewataka wazazi na walezi kuhakikisha watoto wanakwenda shule na kufuatilia mahudhurio yao ili wapate elimu itakayowawezesha kujenga maisha bora ya baadaye.

Wakati huohuo, wananchi walipata fursa ya kuwasilisha kero na changamoto mbalimbali zinazowakabili katika mkutano huo, ambapo wataalamu wa sekta husika walitoa ufafanuzi kuhusu masuala ya barabara, maji, afya, elimu, madini na umeme.

Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kusikiliza wananchi na kutathmini shughuli za kiuchumi zinazofanyika katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Dodoma.

About the author

Alex Sonna