Featured Kitaifa

WAZIRI BITEKO :’ATAKA MADINI KUONGEZA AMANI UKANDA WA MAZIWA MAKUU

Written by mzalendoeditor

Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko akizungumza wakati akifungua Mkutano wa 20 wa Kamati ya Ukaguzi  wa Madini wa  Jumuiya ya Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) ambapo Tanzania  ni mwenyeji wa mkutano huo unaofanyika Mjini Bukoba Mkoa wa Kagera
Mwenyekiti wa Kamati Ukaguzi  wa Madini wa  Jumuiya ya Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) akizungumza  wakati akimkaribisha Waziri wa Madini Dkt. Biteko kuufungua mkutano huo
Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko akiwa na wajumbe  wa Mkutano wa 20 wa Kamati ya Ukaguzi  wa Madini wa  Jumuiya ya Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) ambapo Tanzania  ni mwenyeji wa mkutano huo unaofanyika Mjini Bukoba Mkoa wa Kagera
Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko akiwa na wajumbe  wa Mkutano wa 20 wa Kamati ya Ukaguzi  wa Madini wa  Jumuiya ya Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) ambapo Tanzania  ni mwenyeji wa mkutano huo unaofanyika Mjini Bukoba Mkoa wa Kagera
………………………………………………………….
Na Steven Nyamiti- Kagera
WAZIRI wa Madini, Dkt. Doto Biteko amesema, Kamati ya Ukaguzi wa Madini ya Jumuiya ya Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) ina jukumu kubwa la kuhakikisha kuwa, madini yanayochimbwa katika nchi wanachama wa jumuiya hiyo yanakuwa chachu ya amani na si migogoro.
Dkt.Biteko ametoa rai hiyo leo Aprili 4,2022 wakati akifungua Mkutano wa 20 wa Kamati ya Ukaguzi wa Madini ya Jumuiya ya Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) ambapo Tanzania ni mwenyeji wa mkutano huo unaofanyika mjini Bukoba Mkoa wa Kagera.
“Tunataka tuyaone madini haya yanachangia kwenye kuongeza amani kwenye Ukanda wa Maziwa Makuu, hayachangii vita na mapigano na hayachangii migogoro,” amesema Dkt. Biteko.
ICGLR inaundwa na nchi 12 ambazo ni Angola, Burundi, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya Congo, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Kenya, Uganda, Rwanda, Jamhuri ya Sudan Kusini, Sudan, Tanzania na Zambia.
Amesisitiza kuwa, Tanzania ikiwa miongoni mwa wanachama wa ICGLR itaendelea kuhakikisha madini yanayochimbwa katika nchi zetu hayageuki kuwa nyenzo ya kufadhili uhalifu.
Dkt.Biteko ameeleza kuwa, kikao hicho ni cha Kamati ya Ufuatiliaji wa Madini yanayozalishwa kwenye Ukanda wa Maziwa Makuu ambapo kamati hiyo ina jukumu la kufuatilia madini yanakochimbwa ili kusaidia kuleta faida kwenye nchi husika na kuongeza amani.
Akizungumzia umuhimu wa kamati hiyo amesema, madini ya Bati yanayochimbwa Kyerwa na maeneo mengine ili yaweze kuuzwa kwenye masoko ya nje lazima yawe na cheti cha uhalisia wa kule ulipoyatoa. 
Dkt.Biteko amesema, kama hayana hicho cheti madini hayo hayajulikani na hayawezi kuingia kwenye soko.
Kwa upande mwingine, Dkt. Biteko amesema, mkutano huo ni muhimu kwa Tanzania hususani kwa wachimbaji huku akisisitiza wachimbaji wachimbe kwa kuzingatia Sheria na Utaratibu uliowekwa.
“Serikali imeweka mazingira mazuri sana na Rais wetu anasisitiza kila ambaye anahitaji kuchimba achimbe bila matatizo. Lakini utoroshaji wa madini hauwezi kuvumiliwa,” ameongeza.
Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya Ukaguzi wa Madini ya Jumuiya ya Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR), Fr. Dkt. David Luhaka amesema kuwa, mkutano huo umelenga kuwakutanisha pamoja wakaguzi wa madini wa jumuiya hizo ili kuzungumzia mambo mbalimbali yanayojitokeza na kutolea ufafanuzi.

Aidha, Fr. Dkt. Luhaka amesema kuwa, kamati hiyo itatembelea shughuli za uzalishaji wa madini katika Mkoa wa Kagera ili kujifunza vitu vinavyofanyika katika maeneo hayo na kutoa mapendekezo. 

About the author

mzalendoeditor