Featured Kimataifa

PAPA FRANCIS AWAENZI WANAHABARI WALIOUAWA KATIKA VITA YA UKRAINE

Written by mzalendoeditor

Kiongozi wa kanisa katoliki duniani Papa Francis, Jumapili amewaenzi waandishi wa habari waliouawa katika vita vya Ukraine akisema anatumai Mwenyezi Mungu atawapa malipo kwa kuwatumikia kwa wema watu wote bila kujali ni upande gani wanatokea.

Akizungumza na wanahabari akiwa ndani ya ndege akirejea kutoka Malta, Francis ameeleza kwa mara nyingine kwamba yuko tayari kufanya ziara katika mji mkuu wa Ukraine, Kyiv, lakini akiongeza kuwa hajaamua iwapo hilo litawezekana.

“Nataka kutoa rambirambi kwa wenzenu walioaga dunia, bila kujali upande wanakotokea,” amesema.

“Kazi yenu ni kazi kwa manufaa ya watu wote. Walifariki wakiwa wanafanya kazi kwa ajili ya manufaa ya watu wote kupata habari. Tusisahau kwamba walikuwa na ushujaa. Ninawaombea, ninamuomba Mola awalipe kwa kazi yao.”

Wanahabari sita waliuawa tangu majeshi ya Russia yalipoivamia Ukraine mwishoni mwa mwezi Februari.

Francis amesema pia kwamba amekuwa akipata habari kuhusu Ukraine kwa mawasiliano ya simu kila baada ya siku chache na mwandishi wa habari wa Argentina anayeishi Roma Elisabetta Pique, rafiki yake wa karibu ambaye amekuwa akiripoti vita vya Ukraine tangu mwanzo.

Akiwa njiani kuelekea Malta Jumamosi, Francis alisema safari ya kwenda Kyiv ipo kwenye ratiba.

“Niko tayari kufanya lolote linalowezekana. Vatican inafanya kila kitu kwa upande wa kidiplomasia.

“Kwa sababu za busara na usiri, hatuwezi kutangaza kila kitu hadharani,”, alisema akiwa ndani ya ndege.

About the author

mzalendoeditor