Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na Bunge la Umoja wa Ulaya yamekubaliana kuimarisha
ushirikiano miongoni mwao na miongoni mwa wabunge wao. Hayo yameafikiwa tarehe 02
Aprili 2022 kwenye makao makuu ya Bunge la Umoja wa Ulaya nchini Ufaransa, wakati
wa mazungumzo baina ya Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mhe. Mussa Azzan Zungu na Rais mwenza wa
Bunge la Pamoja la Umoja wa Ulaya na Jumuiya ya Nchi za Afrika, Caribbean na
Pasifiki (OACPS), Mhe. Prof. Carlos Zorrinho).
Mazungumzo hayo yaliyofanyika
pembezoni mwa Mkutano wa 41 wa Bunge la
OACPS na EU ambapo Mhe. Zungu anaongoza
ujumbe wa Tanzania, viongozi hao walikubaliana pia kupitia Mabunge yao
kuhakikisha kuwa uhusiano mzuri uliopo baina ya Tanzania na Umoja wa Ulaya na baina
ya Bunge la Tanzania na Bunge la Umoja
wa Ulaya unaimarishwa zaidi.
Aidha, Mhe. Zungu alitumia fursa
hiyo kumwalika Mhe. Zorrinho pamoja na baadhi ya Wabunge wa Bunge la EU kuitembelea
Tanzania na kujionea wenyewe hatua mbalimbali zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suhuhu Hassan katika kusukuma maendeleo ya
Tanzania. Rais huyo mwenza wa Bunge la Pamoja la Ulaya na ACP alipokea mwaliko
huo kwa furaha na kuahidi kufanya ziara
hiyo nchini siku zijazo akiambatana na baadhi wa Wabunge wa Bunge la Umoja wa
Ulaya. Alieleza kuwa Tanzania ni moja ya nchi za kipaumbele kwa Umoja wa Ulaya
na Bunge hilo linafurahishwa na hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Tanzania kusimamia
ajenda za maendeleo na ustawi wa jamii, hususan katika kuboresha mazingira ya
uwekezaji na kuimarisha demokrasia na haki za binadamu.
Mhe. Zungu alimwomba
mwenyeji wake huyo kuwahamasisha wawekezaji wa Ulaya waendelee kuja kuwekeza
nchini kwenye masuala ya uchimbaji wa gesi na maeneo mengine, kwani Tanzania imebarikiwa
kuwa na fursa nyingi za uwekezaji.
Viongozi hao walihitimisha mazungumzo
yao kwa kusisitiza umuhimu wa kuongeza ushawishi wa mabunge yao kutoa miongozo
itakayoimarisha ushirikiano baina ya Umoja wa Ulaya na nchi za Afrika,
Carribean na Pacific pamoja na masuala yanayohusu kukabiliana na mabadiliko ya
tabianchi na kuimarisha amani eneo la ukanda wa maziwa makuu hususan nchini
Msumbiji. Professa Zorrinho alieleza kuwa EU ina imani kubwa zaidi na Tanznaia
katika masuala ya usuluhishi wa migogoro na kukuza amani duniani.
Katika
mazungumzo hayo, Mhe. Zungu aliambatana na Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji
na kwenye Umoja wa Ulaya, Mhe. Jestas Abuok Nyamanga na maafisa wengine
waandamizi wa Ubalozi na Bunge.
Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa |
Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Mussa Assan Zungu (aliyesimama kulia) akibadilishana mawazo na mmoja wa Wabunge wa Bunge |