Featured Kitaifa

KINABABA WATAKIWA KUONGOZANA NA WAKE ZAO KLINIKI

Written by mzalendoeditor

Baba ana umuhimu sana kumsindikiza mama kliniki

Na. Zillipa Joseph, Katavi

Kinababa wameshauriwa kuongozana na wake zao kliniki pale mama anapokuwa mjamzito kwa ajili ya kufahamu maendeleo ya mtoto aliyeko tumboni.

Ushauri huo umetolewa na Mratibu wa afya ya mama na mtoto mkoa wa Katavi Sista Elida Machungwa wakati akifanya mahojiano maalum na mwandishi wa habari.   

‘Ingawa akina baba walio wengi sasa wanajua umuhimu wa kuwasindikiza wazazi wenza (akina-mama) kliniki wakati wa ujauzito na hata baada ya kujifungua, bado wapo wengi wanadhani kuwa wanatakiwa kwenda huko kwa ajili ya kupima ukimwi tu’ alisema.

Amesema hivyo si sawa kwani kliniki yanafanyika mambo mengi ambayo pia ni faida kwa baba na yatasaidia  katika makuzi na malezi ya mtoto.

‘Sote tunawajibika katika makuzi ya mtoto, kwahiyo ni wajibu wa mwenza kumsindikiza mwenzake kwani hilo litaleta ukaribu pia kati ya baba na mtoto aliyeko tumboni’ alisisitiza.

Amesema tafiti zinaonyesha kuwa mtoto hushiriki furaha aliyonayo mamaambapo mama mwenye furaha, na mtoto naye anakuwa na furaha angali tumboni.

Wakizungumzia suala la makuzi na malezi wakinababa walio wengi wamedai kukosa nafasi ya kuongozana na wake zao kliniki kutokana na kubanwa na majukumu ya kila siku ya kutafuta riziki.

Sebastian Haule ni mkazi wa manispaa ya Mpanda amesema yeye ana watoto wanne na hajawahi hata mara moja kumsindikiza mke wake kliniki.

‘Haya mambo ni ya kisasa mimi naona yanasisitizwa sasa zamani wala kulikuwa hakuna mambo ya kufuatana fuatana’ alisema

Akizungumzia umuhimu wa kukaa na watoto alisema umuhimu upo kwani unamwezesha baba kufahamu tabia ya watoto wake na kukiri kuwa kwa kazi zake mara nyingi amekuwa akikaa na familia wakati wa jioni tu.

Kwa upande wao baadhi ya wanawake wamesema wanajikia faraja pale baba anapomsindikiza kliniki.

About the author

mzalendoeditor