Featured Kitaifa

WAZIRI MBARAWA  AWAONYA WATENDAJI WA BANDARI YA DAR ES SALAAM 

Written by mzalendoeditor

Waziri  wa Ujenzi na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa wa  kwanza kulia akimwelekeza jambo mkurugenzi wa Usimamizi wa Mitambo   Mhandisi Pius Kayuni, Baada ya  Waziri Mbarawa kufanya ziara Usiku katika Bandari ya Dar es Salaam na kubaini baadhi ya Mitambo katika Bandari  hiyo ya kushusha na kupakia Makasha ni Mibovu.

Mmoja ya Meli kubwa ikiwa imetia nanga katika Bandari ya Dar es Salaam  jana Usiku tayari  kwa kupakia na Kushusha Makasha .

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa akiwa ameshika file linaoonyesha Mitambo inayofanyiwa Matengezo  katika kalakana ya Bandari jijini Dar es Salaam na kubaini Mitambo mingi imekaa muda Mrefu bila kufanyiwa Matengenezo

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi wa tatu kutoka kulia akiangalia baadhi ya vipuri vya Mitambo katika Kalakana ya Bandari jijini Dar es Salaam  baada ya kufanya ziara usiku katika bandari hiyo.

………………………………………………………

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, ameuagiza uongozi wa Bandari ya Dar es Salaam kutonunua mitambo yoyote kutoka kwenye kampuni ya Port Marine Solution kwani kumeisababishia hasara kwa Serikali kutokana na kutofanya kazi kama ilivyokusudiwa.

Prof. Mbarawa ametoa kauli hiyo baada ya ziara ya kushtukiza majira ya usiku katika Bandari ya Dar es Salaam ili kujionea utendaji kazi wa mitambo ya kushusha na kupakia makasha na kubaini vifaa na mitambo iliyonunuliwa kutoka kwenye kampuni hiyo  havifanyi kazi vizuri na vingine ni vibovu. 

“Mtambo huu umenunuliwa  miaka miwili iliyopita lakini kwa mwaka 2021 umefanya kazi kwa siku 126 tu kati ya siku 365 na hivyo kuisababishia hasara Serikali”, amesema Mbarawa. 

Aidha,  Waziri Mbarawa ameutaka uongozi wa TPA na kitengo cha kushusha na kupakia makasha katika bandari ya hiyo kuhakikisha wanaondoa makasha yote yaliyokaa muda mrefu katika Bandari hiyo na kuyahamishia katika Bandari kavu ya Kwala na Ubungo. 

“Natoa wiki mbili kwa TPA na TICTS kuhakikisha makasha yote yaliyokaa hapa kwa muda mrefu yanaondolewa haraka sana na nafahamu kuwa TPA mna makasha 115 na TICS makasha 400,” amesisitiza Mbarawa. 

Kwa upande wake, Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam, Eng. Juma Kijavara, ameahidi kuyafanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa na Mheshimiwa Waziri ili kuendelea kuboresha utoaji huduma wa Bandari ya Dar es Salaam. 

Awali akitoa taarifa ya mitambo, Msimamizi wa Mitambo katika Bandari ya Dar es Salaam, Mhandisi Pius Kayuni, amemweleza waziri kuwa mitambo hiyo ilinunuliwa ikiwa mipya na ilifanyiwa majaribio na ilionekana ipo vizuri lakini kwenye utendaji kazi inasuasua. 

About the author

mzalendoeditor