Featured Kitaifa

LAAC YARIDHISHWA NA KASI YA UJENZI WA SOKO KUU LA KISASA NA STENDI KUU NYEGEZI JIJINI MWANZA

Written by mzalendoeditor

Na Asila Twaha, Mwanza

Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Hesabu za Serikali za Mitaa(LAAC) imeridhishwa na kasi ya ujenzi wa soko kuu la kisasa na Stendi iliyopo Kata ya Nyegezi, jijini Mwanza.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Selemani Zedi ametoa kauli kwenye ziara ya Kamati hiyo ya kukagua wa miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza ambapo leo kamati hiyo imekagua ujenzi wa Soko na Stendi hiyo.

Mhe. zedi amesema, ushirikiano mzuri ulipo katika Halmashauri hiyo umeonesha maendeleo mazuri ya miradi yote waliokagua jinsi inavyoendelea.

“Tumeridhishwa na kasi ya ujenzi na thamani iliyopo lakini pia kuwepo na mafundi na vifaa imeonesha dhahiri miradi hii itamalizika kwa muda uliopangwa na wananchi kuweza kupata huduma mapema,”amesema.

Mhe. Zedi amemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel kwa usimamizi mzuri wa miradi na kuendelea kumuomba kuendelea na ushirikiano na usimamizi kwa kuleta matokeo mazuri kwa miradi na fedha za Umma zinazopelekwa kwenye Jiji hilo.

Aidha, amewashauri watendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuwajibika kwenye majukumu yao ili kuwa na maendeleo chanya katika utoaji wa huduma kwa jamii.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel amesema, maelekezo yote ya kamati wamepokea na wataendelea kushirikiana na kusimamia fedha zote za miradi zinazopelekwa katika Jiji hilo zinatumika kwa kufuata sheria, na thamani ya miradi ionekane kwa manufaa ya wananchi.

Katika hatua nyingine, Kamati hiyo imekagua wodi ya wanaume katika Hospitali ya Halmashauri ya Jiji la Mwanza na kuupongeza uongozi kwa kuongeza fedha za mapato ya ndani katika kukamilisha hospitali hiyo na hasa kununua vitanda na vifaa vyingine ili kuanza kutoa huduma.

“Nishauri hospitali nyingine ziangalie uwezekano wa mapato yao kwa kuona uwezekano wakupata vifaa kuna Halmashauri nyengine majengo ya hospitali yamekamilika ila hata vifaa vidogo wanashindwa kununua nishauri angalieni uwezekano ili hospitali zilizokamilika wananchi wapate huduma,” Mhe. Zedi

About the author

mzalendoeditor