Uncategorized

KAMATI YA BUNGE YAISHAURI TEMESA KUJIENDESHA KIBIASHARA

Written by mzalendoeditor

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Selemani Kakoso, akishauri jambo kwa watendaji wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), hawapo pichani, wakati Kamati hiyo ikikagua miradi ya ukarabati wa vivuko vya MV. Sabasaba na MV. TEMESA jijini Mwanza. Kulia kwake ni Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Godfrey Kasekenya.

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, akisikiliza jambo kutoka kwa Naibu Katibu Mkuu Ujenzi, Ludovick Nduhiye, wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu ikikagua mradi wa ukarabati wa Karakana ya Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) jijini Mwanza. Kulia ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo Selemani Kakoso (Mb).

Mkurugenzi wa Huduma za Matengenezo na Ufundi, kutoka Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), Mhandisi Hassan Karonda, akifafanua jambo kwa Wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Miundombinu, wakati kamati hiyo ikikagua mradi wa ukarabati wa Karakana ya TEMESA jijini Mwanza.

Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, wakiwa kwenye picha ya pamoja ndani ya Kivuko cha MV. TEMESA, kinachokarabatiwa jijini Mwanza. Wa nne kulia ni Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Godfrey Kasekenya.

Picha na WUU

……………………………………………….

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Mheshimiwa Seleman Kakoso (Mb), amewaongoza wajumbe wa kamati hiyo, kukagua miradi ya ukarabati wa  karakana na vivuko inayosimamiwa na Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), jijini Mwanza na kuushauri Wakala huo kujiendesha kibiashara.

Kamati hiyo imekagua mradi wa ukarabati wa Karakana ya TEMESA mkoa wa Mwanza unaogharimu Shilingi Milioni 500.7, ambao utekelezaji wake umefikia asilimia 70 na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Aprili mwaka huu, ambapo hadi sasa tayari Mkandarasi wa mradi huo ameshalipwa kiasi cha shilingi Milioni 300.

Wakizungumza katika kikao cha majumuisho wajumbe wa Kamati hiyo ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu wameishauri TEMESA kujitathmini na kuweka mikakati ya kujiendesha kibiashara sambamba na kununua vitendea kazi vya kisasa vya karakana, kuajiri mafundi wenye ujuzi, kununua vipuri vya kutosha, na kukamilisha kazi za wateja kwa kuzingatia ubora na ndani ya muda stahiki.

“Mtendaji Mkuu ibadilishe TEMESA ili iweze kujiendesha, Serikali imewekeza fedha nyingi kwenye Wakala huu, na hivyo ni vizuri ukaajiri mafundi wa kutosha na wenye ujuzi, sambamba na kuboresha mazingira ya utendaji kazi ili TEMESA iweze kutoa huduma inayolingana na thamani ya fedha zinazotolewa na wateja wake.” ameshauri Kakoso.

Vile vile kamati hiyo imekagua mradi wa ukarabati wa kivuko cha MV. Sabasaba unaogharimu Shilingi Milioni 239.9, ambapo hadi sasa Mkandarasi ameshalipwa kiasi cha shilingi milioni 150, pamoja na mradi wa ukarabati wa kivuko cha MV. TEMESA kinachotoa huduma kati ya Kirumba na Luchelele jijini Mwanza. Vivuko hivi vyote vinakarabatiwa na Kampuni ya Songoro Marine Boatyard ya jijini Mwanza

Wajumbe hao wameonyesha kufurahishwa na Mkandarasi huyo wa Kitanzania kwa kutekeleza miradi ya ukarabati wa vivuko pamoja na ujenzi wa vivuko vipya. Hata hivyo, wameishauri TEMESA kuhakikisha kuwa Mkandarasi huyo anasimamiwa kwa karibu ili aweze kufanya kazi nzuri zaidi.   

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Godfrey Kasekenya, ameiambia Kamati hiyo kuwa kivuko cha MV. Sabasaba kinatarajiwa kupelekwa katika eneo la Kigongo – Busisi kama kivuko mbadala ili kivuko cha MV. Misungwi kifanyiwe ukarabati mkubwa na baadae kivuko cha MV. Sabasaba kitapelekwa kuongeza nguvu katika eneo la Nyakaliro – Kome.

Nae Naibu Katibu Mkuu Ujenzi, Ludovick Nduhiye ameiambia Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuwa Wizara itaendelea kuisimamia TEMESA na kuhakikisha kuwa maagizo yote yanayotolewa na kamati hiyo yanatekelezwa kikamilifu ndani ya muda ulioainishwa.

Awali akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi ya TEMESA jijini Mwanza, Mtendaji Mkuu TEMESA Lazaro Kihalala, ameiambia Kamati hiyo kuwa ukarabati wa Karakana ya Mwanza umelenga kuboresha mazingira ya utendaji kazi kwenye karakana hiyo. Aidha, ameahidi kuwa ofisi yake itaandaa taarifa za kina za utekelezaji wa miradi wanayoisimamia na kuiwasilisha kwenye kikao cha kamati hiyo Bungeni jijini Dodoma.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu iko jijini Mwanza kwa ajili ya kukagua miradi mbali mbali ya Serikali inayotekelezwa jijini humo.

About the author

mzalendoeditor