Uncategorized

KAMATI YA BUNGE YAAGIZA MKAKATI MATUMIZI YA STENDI KUU YA MABASI NJOMBE

Written by mzalendoeditor

Na. Silvia Hyera, Njombe

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa imemtaka Mkuu wa Wilaya ya Njombe na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Njombe kushirikiana kwa pamoja katika kuandaa mkakati ambao utaimarisha matumizi ya Stendi Kuu ya Halmashauri ya Mji wa Njombe kwa kuhakikisha shughuli zote za usafirishaji zinafanyika katika stendi hiyo na sio katika stendi ya zamani.

Akizungumza kwa niaba ya kamati hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa , Mhe.Grace Tendega amesema uwepo wa matumizi ya stendi ya zamani unahatarisha usalama wa wananchi kutokana na eneo iliyopo, lakini pia inazorotesha ukusanyaji wa mapato katika Halmashauri ya Mji wa Njombe.

Hayo yamebainishwa Februari 17, 2022 katika ziara ya kamati katika Halmashauri ya Mji Njombe baada ya kugundua kuwa, shughuli za usafirishaji bado zinaendelea katika stendi ya zamani badala ya stendi kuu ya mabasi kama ilivyoagizwa.

Sambamba na hilo, Mhe. Tendega ameipongeza Halmashauri ya Mji wa Njombe kwa ujenzi wa soko la kisasa ambalo linajumuisha biashara mbalimbali, kutokana na ukubwa wa soko hilo amemshauri Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kuhakikisha soko hilo linakatiwa bima, lakini pia uwepo wa vifaa vya kuzimia moto.

Aidha, amemtaka kuboresha miundombinu ya vyoo ili kudhibiti maambukizi ya magonjwa mbalimbali, akisisitiza kutokana na msongamano wa watu wengi matumizi ya vyoo vya kukaa unahatarisha afya za watumiaji.

Naye Mhe. Conchesta Rwamulaza ambaye ni mjumbe wa kamati hiyo amemshauri Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Njombe kuhakikisha anasimamia vizuri ukusanyaji wa mapato ili halmashauri hiyo iweze kujitegemea yenyewe na kuondokana na utegemezi kutoka Serikali Kuu.

Katika Halmashauri ya Njombe kamati hiyo imetembelea na kufanya ukaguzi katika Stendi Kuu ya mabasi na ujenzi wa Soko Kuu, ambapo miundombinu hiyo imejengwa kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri pamoja na Programu ya Uimarishaji Mamlaka za Miji (ULGSP) inayofadhiliwa na Serikali kupitia Benki ya Dunia.

About the author

mzalendoeditor