Featured Kitaifa

RAIS SAMIA ATOA AGIZO LA KUANDAA KANUNI ZA MIKUTANO YA VYAMA VYA SIASA

Written by mzalendoeditor

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Wajumbe wa Kikosi Kazi cha Kuratibu Maoni ya Wadau wa Demokrasia ya Vyama vingi vya Siasa leo tarehe 12 Machi, 2022, Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma

……………………………………………………..

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ametoa agizo kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Bunge kuandaa kanuni zitakazoelekeza jinsi ya kufanya mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa.  

Rais Samia ametoa maelekezo hayo baada ya kupokea maazimio ya awali kutoka Kikosi kazi alichokiteua cha kufuatilia hoja zilizojitokeza katika mkutano wa wadau wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa uliofanyika jijini Dodoma Desemba 15 hadi 17.

Rais Samia amemwagiza Waziri huyo wa wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Bunge kushirikiana na Tanganyika Law Society (TLS) pamoja na Zanzibar Law Society (ZLS) kutengeneza kanuni hizo. 

Kikosi kazi hicho chenye wajumbe 24, na ambacho kinawajibika moja kwa moja kwa Mhe. Rais, kiliwasilisha maazimio hayo Ikulu Jijini Dodoma. Maazimio hayo yamegawanyika katika makundi matatu ya muda wa utekelezaji.

Azimio la muda mfupi ni uandaaji wa kanuni zitakazoelekeza jinsi ya kufanya mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa.  

Baadhi ya maazimio ya muda wa kati ni pamoja na Rushwa na maadili katika uchaguzi, Ruzuku, Elimu ya uraia, huku masuala yanayohusu Uchaguzi na Katiba mpya vikiwa ni mpango wa muda mrefu.

About the author

mzalendoeditor