Featured Kitaifa

KATIBU MKUU AFYA ATAKA USHIRIKIANO KATIKA MAENEO YA UTOAJI HUDUMA

Written by mzalendoeditor

Na WAF – DSM.

KATIBU MKUU Wizara ya Afya, Prof. Abel Makubi amewataka Watumishi Wizara ya Afya kuimarisha ushirikiano na uhusiano katika maeneo ya utoaji huduma ili kuleta tija katika utoaji wa huduma kwa mwananchi.

Prof. Makubi ameyasema hayo Jijini Dar es salaam wakati akifungua mafunzo ya huduma kwa mteja yaliyohudhuriwa na Wakurugenzi, Wakuu wa Idara na Vitengo,Wasajili wa Mabaraza na bodi za kitaalamu pamoja na baadhi ya Watumishi kutoka Wizara ya Afya.

“Mahusiano na ushirikiano kazini ni kitu kizuri, lakini pia hata katika jamii inayokuzunguka ni vizuri kuwa na mahusiano mazuri kwasababu lengo ni kujenga nyumba moja ili kuleta tija katika kuboresha Sekta ya afya sio kuharibu.”

Amesema, unapokuwa na mahusiano mazuri katika maeneo yote husaidia hata mambo ya kijamii yakafanikiwa ndani na nje ya ofisi.

Sambamba na hilo Prof. Makubi ametoa wito kwa Watumishi kutafuta njia bora ya kutatua misuguano baina ya mtu na mtu ili kuepuka kutengeneza misuguano zaidi katika maeneo ya kutolea huduma jambo ambalo hupelekea kupunguza ufanisi katika maeneo ya kazi.

“Tujifunze kutatua matatizo kwa kuanza sisi wenyewe, kila mmoja anamapungufu hakuna aliye msahihi asilimia 100%.” Amesema.

Aidha, amewataka Watumishi kuwa wazalendo kwa kufanya kazi kwa bidii na ubunifu ili kuboresha huduma kwa wananchi, huku akisisitiza suala la utunzaji siri kama maadili ya utumishi yanavyoelekeza.

Mbali na hayo, Prof. Makubi amewapongeza Watumishi na Viongozi wote wa Wizara ya Afya kwa jitihada kubwa wanazoendelea kufanya katika kuboresha utoaji wa huduma kwa Wananchi, hasa katika kipindi hiki cha mwaka mmoja wa Rais Samia ambapo mambo makubwa yamefanyika ili kuboresha huduma.

Hata hivyo Prof. Makubi amesema, Serikali imeboresha sana upatikanaji wa vifaa na vifaa tiba na uboreshaji wa miundombinu ya kutolea huduma hivyo kuwaelekeza Wakurugenzi kusimamia utoaji huduma bora ili kuwe na uhusiano kati ya ubora wa miundombinu na ubora wa huduma katika maeneo ya kazi.

Amesisitiza kuwa, Serikali kupitia Wizara ya Afya imedhamiria kuboresha huduma kwa Wateja, huku akisisitiza, “huduma kwa mteja ni neno pana, linaanzia mgonjwa anapoingia getini, kuelekea mapokezi, kuonana na Wataalamu mpaka anatoka”.

About the author

mzalendoeditor