Featured Kitaifa

MWANAFUNZI DARASA LA SITA AJERUHIWA NA FISI AKIENDA SHULENI

Written by mzalendoeditor

Mwanafunzi wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Somanda A iliyopo Halmashauri ya Mji wa Bariadi mkoani Simiyu, Hollo Malugu (14) ameng’atwa na fisi wakati akielekea shuleni na kumjeruhi vibaya kichwani.

Tukio hilo limetokea leo majira ya saa moja asubuhi wakati mtoto huyo akielekea shuleni, ambapo akiwa barabarani ghafla fisi huyo alitokea katika milima iliyopo kwenye mtaa huo kisha kuanza kumshambulia mtoto huyo.

Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Bariadi, Dkt. Judith Ringia akiongea na waandishi wa habari amethibitisha kupokelewa kwa mtoto huyo katika hospitali ya halmashauri hiyo kwa ajili ya matibabu.

Dkt. Ringia amesema kuwa mtoto huyo amejeruhiwa vibaya maeneo ya kichwani , ambapo fisi alimng’ata na kunyofoa nyama huku akibainisha madaktari na wahudumu walifanya jitihada za haraka kumpatia huduma ya kwanza.

“ Ni kweli mtoto aliletwa hapa akiwa na hali mbaya na ameng’atwa kichwani na kunyofolewa baadhi ya nyama, alipofikishwa hapa hospitali tulimpatia huduma ya kwanza, lakini imeonekana hali yake kuwa mbaya tumempatia rufaa apelekwe Bugando mkoani Mwanza,” amesema Dkt. Ringia.

Mama mzazi wa mtoto huyo, Mwasi Sumbuka, amesema kuwa katika mtaa wao kumekuwepo na fisi wengi ambao wanatokea kwenye Pori la Magereza la mjini Bariadi, ambapo mtoto wake alivamiwa wakati akielekea shuleni.

“Wakati anaenda shule, njiani ndipo akavamiwa na akaanza kupiga kelele, ndipo wananchi ambao nao walikuwa njiani wakajitokeza na kumuokoa, lakini tayari alikuwa amemjeruhi sana kichwani, ndipo na mimi nikamkuta akiwa na hali mbaya damu zikimwagika,” amesema.

Mahega Mpango, mmoja kati ya wasamaria wema aliyemwokoa mwanafunzi huyo, amesema kuwa bila yeye mtoto huyo angepoteza maisha kwani fisi alikuwa amemkandamiza chini huku mtoto huyo akiwa anapiga kelele.

“Baada ya kusikia kelele nikakimbia kumuokoa mtoto, ndipo nikakuta fisi akiwa amemkandamiza mtoto chini huku akimg’ata kichwani, nikachukua mawe na kuanza kumpiga ndipo akakimbia,” amesema Mpango.

About the author

mzalendoeditor