Featured Kitaifa

NSSF YASHIRIKI MAADHIMISHO SIKU YA WANAWAKE DUNIANI

Written by mzalendoeditor

Watumishi  Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF)  wakipita kwa mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka wakati wa maadhimisho ya Siku ya wanawake duniani yaliyofanyika leo March 08, 2022 ambapo kimkoa yamefanyika wilaya ya Chemba mkoani Dodoma.

Watumishi  Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF)  wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kushiriki maadhimisho ya siku ya wanawake duniani ambapo kimkoa yamefanyika wilaya ya Chemba mkoani Dodoma.

MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka,akizungumza wakati wa Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambapo katika Mkoa wa Dodoma yamefanyika Wilaya ya Chemba leo March 8,2022

………………………………………..

MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka amewataka wanawake wa mkoa huo kujenga jamii yenye usawa ili watoto wa kike na kiume waweze kujisimamia katika maisha yao.

RC Mtaka amesema ni lazima wazazi wafundishe watoto wao masuala ya kijinsia ili kujenga jamii iliyo bora.

Ameyasema hayo leo Machi 8, 2022 wakati wa Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambapo katika Mkoa wa Dodoma yalifanyika katika Wilaya ya Chemba.

Akizungumzia kuhusu manyanyaso ya wanawake katika jamii, RC Mtaka amesema ni lazima yaondolewe ili kusaidia wanawake kutekeleza majukumu yao katika jamii.

Pia, Mtaka ameongeza kuwa, Mkoa wa Dodoma utaandaa siku maalum kwa ajili ya kutambua wanawake wanaothubutu katika jamii ili waweze kutoa elimu ya mafanikio yao kwa wanawake wenzao.

Wakati huo huo, RC Mtaka pia amekabidhi vyeti vya pongezi na tuzo kwa watoto wa kike waliofanya vizuri darasani, wanawake mashuhuri na watoto waliofanya vizuri masomo ya Sayansi katika Chuo cha DECA.

Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Neema Majule amewataka wanawake wasimame imara katika kufanya kazi. Amesema, wanawake wanaweza kufanya mabadiliko makubwa ili waweze kujikwamua kiuchumi.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Munkunda amesema, wanawake waoneshe ulimwengu ujuzi wao kupitia fursa mbalimbali katika jamii.

“Wanawake tunaweza kufanya mambo makubwa kwa sababu sisi ni viongozi. Tukipewa kazi hatuharibu kwa sababu tumezaliwa kuwa viongozi,” amesema Mkuu huyo wa wilaya.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya mwenyeji wa Chemba Saimon Chacha akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Chemba amepongeza uongozi wa Mkoa wa Dodoma kwa kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani katika Wilaya ya Chemba.

Ameongeza kuwa, Halmashauri ya Chemba inatoa mikopo kwa wanawake pamoja na elimu ya mambo mbalimbali ili kuweza kuwasaidia wanawake katika jamii.

Maadhimisho ya Siku ya Wanawake 2022 yamepambwa na kaulimbui isemayo “Kizazi cha Haki na Usawa kwa Maendeleo Endelevu”.

About the author

mzalendoeditor