Featured Kitaifa

WATANZANIA WAASWA KUPIMA AFYA ZAO

Written by mzalendoeditor

MWENYEKITI wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maswala ya Ukimwi, Kifua Kikuu, Madawa ya Kulevya na Magonjwa yasiyoambukiza,Mhe. Fatma Toufiq,akizungumza katika kikao na uongozi wa Mkoa wa Mara wakati wa ziara ya kamati hiyo ya kutembelea  Mgodi wa North Mara.

Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe.Ally Hapi,akizungumza wakati wa ziara ya  Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maswala ya Ukimwi, Kifua Kikuu, Madawa ya Kulevya na Magonjwa yasiyoambukiza, ya kutembelea  Mgodi wa North Mara,uliopo Mkoani Mara. 

Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Bw. Tumaini Macha,akizungumza  wakati wa ziara ya  Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maswala ya Ukimwi, Kifua Kikuu, Madawa ya Kulevya na Magonjwa yasiyoambukiza, ya kutembelea  Mgodi wa North Mara,uliopo Mkoani Mara.

Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maswala ya Ukimwi, Kifua Kikuu, Madawa ya Kulevya na Magonjwa yasiyoambukiza wakifatilia mada mbalimbali wakati wa ziara ya kutembelea  Mgodi wa North Mara,uliopo Mkoani Mara. 

MWENYEKITI wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maswala ya Ukimwi, Kifua Kikuu, Madawa ya Kulevya na Magonjwa yasiyoambukiza,Mhe. Fatma Toufiq,akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kumaliza kukagua  Mgodi wa North Mara,uliopo Mkoani Mara. 

…………………………………………………..

NA. Majid Abdulkarim, MARA

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Maswala ya Ukimwi, Kifua Kikuu, Madawa ya Kulevya na Magonjwa yasiyoambukiza, imewataka watanzania kujitokeza kupima afya zao katika vituo vya kutolea huduma za afya.

Rai hiyo imetolewa leo mkoani Mara na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Fatma Toufiq, wakati kamati hiyo ilipotembelea Mgodi wa North Mara, ambapo ameutaka uongozi wa Mkoa kufanya uhamasishaji kwa jamii ili kujitokeza kupima afya zao hali itakayowasaidia kuishi kwa malengo.

Mhe. Toufiq amesema kuwa, elimu ya uhamasishaji ya upimaji afya, ikitolewa kwa jamii wakapata uelewa wa umuhimu wa kupima afya kutasaidia kujua afya zao na watakao gundulika kuwa na mambukizi wataanzishiwa dawa mara moja.

“Pima afya Ishi kwa malengo, wasio pima wanaishi kwa matumaini maana yake hujui hali ya afya yako, jambo linalomfanya mtu kuishi na wasiwasi juu ya afya yake”, amesisitiza Mhe. Toufiq.

Mhe. Toufiq ameongeza kuwa, hakuna sababu ya kuogopa kupima afya yako kwa sababu dawa zipo, na kwamba iwapo utagundulika kuwa na maambukizi utaanzishiwa dawa.

Amewataka pia wataalamu wa afya nchini kuendelea kuhamasishana katika maeneo yao ya kazi, kujitokeza kupima afya zao ili kuleta ufanisi mzuri katika utendaji kazi wao kuliko kuishi kwa matumaini.

“Wanaume mjitokeze kwa wingi kwenda kupima kwa sababu taaarfa zinaonyesha wanaume wengi mnategemea matokeo ya wanawake zenu na nyie hamjitokezi kupima afya zenu”, amesisitiza Mhe. Toufiq.

Aidha Mhe. Toufiq ameendelea kusema kuwa, mkoa huo unakila sababu ya kuendelea kutoa elimu kwa wale wanaoendelea kupata ujauzito kwenda kupima haraka na kujua afya zao ili watoto watakao zaliwa wasiweze kupata maambukizi yoyote.

Ameeleza kuwa elimu ikitolewa mapema juu ya watu kujitokeza kupima afya zao, kutaongeza uwezekano wa kuzuia maambukizi ya virusi vya ukimwi wakati wa wakuzaliwa kwa watoto.

Pia Mhe. Foufiq amezungumzia ugonjwa wa kifua kikuu, ambapo amesema, tunakila sababu ya kuhamasisha watu kujitokeza kupima ugonjwa huo, kwa kuwa dawa zipo na unatibika

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Bw. Tumaini Macha, amesema, Mkoa Mara mwaka 2021/22 ulitenga jumla ya Tsh 16,863,499,463.35 kwa ajili ya sekta ya Afya ambapo jumla ya Tsh 1,178,212,163.03 (7%) zilitengwa kwa ajili ya kutekeleza afua za mapambano dhidi ya VVU.

Amesema moja ya malengo ya serikali ni kutekeleza mpango wa Taifa wa kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma (NTLP) ambao ni mpango mkakati wa miaka minne (IV) wa Afya nchini kote

“Serikali inaendelea kutekeleza malengo yote ya mkakati wa mapambano dhidi ya magonwa ya Kifua kikuu na Ukoma kwa kuzingatia mpango wa Taifa wa kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma (NTLP) na mpango mkakati wa miaka minne (IV) wa Afya “, ameeleza Bwana Macha.

Bw. Macha ameongeza kuwa, serikali ina mikakati ya kuzuia maambukizi mapya, kuongeza ugunduzi wa wagonjwa wapya wa Kifua Kikuu kwa kutoa matibabu stahiki kwa wale watakaobainika kuwa na ugonjwa wa Kifua Kikuu kwa kuendelea kuwakinga na kudhibiti ugonjwa kuendelea kusambaa kwa watu wengine.

About the author

mzalendoeditor