Featured Kitaifa

DC SERERA AKABIDHI CHAKULA KWA WANAFUNZI SIMANJIRO

Written by mzalendoeditor

Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Dk Suleiman Serera akizungumza baada ya kukabidhi tani 50.7 za mahindi, tani 27.6 za maharage na lita 2,220 za mafuta ya kupikia iliyotolewa na shirika la World Vision Tanzania kwa wanafunzi wa shule tisa za msingi na sekondari za Tarafa ya Ruvu Remit kitakachotumika kwa muda wa miezi mitatu.

Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Dkt Suleiman Serera (kulia) akiwakabidhi wanafunzi wa shule ya msingi Ngage, moja kati ya tani 50.7 za mahindi, tani 27.6 za maharage na lita 2,220 za mafuta ya kupikia iliyotolewa na shirika la World Vision Tanzania kwa wanafunzi wa shule tisa za msingi na sekondari za Tarafa ya Ruvu Remit kitakachotumika kwa muda wa miezi mitatu.

…………………………………………………………….

Na Mwandishi wetu, Simanjiro

Shirika la World VisionTanzania limetoa msaada wa chakula kwa shule tisa za msingi na sekondari za Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara kitakachotumika kwa muda wa miezi mitatu.

Msaada huo wa chakula uliotolewa ni tani 50.7 za mahindi, tani 27.6 za maharage na lita 2,220 za mafuta ya kupikia kwa shule tisa za Msingi na sekondari za Tarafa ya Ruvu Remit.

Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Dkt Suleiman Hassan Serera amesema msaada huo wa chakula utatumiwa na wanafunzi wa shule saba za msingi na shule mbili za sekondari za Tarafa ya Ruvu Remit.

Dkt Serera amelishukuru shirika la World Vision Tanzania kwa kutoa chakula hicho ambacho kitatumiwa na wanafunzi hao kwa muda wa miezi mitatu ya Machi, Aprili na Mei.

Amesema wazazi wengi wa eneo hilo wanatokana na jamii ya wafugaji ambao waliathirika mno na ukame uliotokea mwaka jana na kusababisha mifugo mingi kufa na kuwapunguzia ukwasi wa kuchangia chakula hicho.

“Mchango huu umetolewa katika kipindi hiki ili kusaidia nguvu za wazazi kuchangia upatikanaji wa chakula mashuleni hivyo tunawashukuru mno shirika hilo kwa kufanya jambo hili,” amesema Dkt Serera.

Amesisitiza chakula hicho kutumika kwao makusudi yaliyotolewa na wazazi wajipange ipasavyo kuendelea na wajibu wao kabla ya chakula hicho hakijaisha.

“Sisi Simanjiro tunaamini upatikanaji wa chakula cha uhakika mashuleni utachochea ufaulu ipasavyo kwa wanafunzi kusoma wakiwa wameshiba,” amesema Dkt Serera.

Mwanafunzi wa shule ya msingi Ngage James Loishiye amesema ni vyema wanapokula shuleni kuliko kutembelea umbali mrefu wa kula nyumbani na kurudi shule.

Loishiye amewashukuru World Vision Tanzania kwa kuwajali wanafunzi wa eneo hilo kwani chakula hicho kitawasaidia kwa muda huo wa miezi mitatu watakapotumia.

About the author

mzalendoeditor