Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti akizungumza kwenye kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) jana mjini Sumbawanga ameagiza viongozi wa vijiji,mitaa na kata kutoa elimu ya umuhimu wa anwani za makazi na postikodi.

Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Dkt. Boniface Kasululu (aliyesimama)  akitoa maelezo ya awali ya zoezi la postikodi na anwani za makazi kwa wajumbe wa kikao cha kamati ya ushauri mkoa wa Rukwa jana.

Mkuu wa Wilaya ya Kalambo Tano Mwera (kushoto) akiwa kwenye kikao cha Kamati ya Ushauri Mkoa wa Rukwa jana mjini Sumbawanga.

Mbunge wa Nkasi Kaskazini Aida Khenani akichangia jana kuhusu umuhimu wa kuweka vipaumbele vya miradi ya maendeleo wakati wa kikao cha Kamati ya Ushauri (RCC) mkoa wa Rukwa jana. Wa kwanza kushoto ni Mbunge wa Sumbawanga Mjini Aeisi Hilary (aliyekaa).

Katibu Tawala Msaidizi Mipango na Uratibu Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa David Kilonzo akiwasilisha taarifa ya utekelezaji bajeti ya mwaka 2021/22 na mpango wa bajeti wa mwaka 2022/23 jana mjini Sumbawanga.

Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Jonas Kilima akitoa mada kuhusu utekelezaji wa mfumo wa uwekaji wa anwani na postikodi jana kwenye kikao cha Kamati ya Ushauri ( RCC) mjini Sumbawanga.

Wajumbe wa Kikao cha Kamati Ushauri mkoa wa Rukwa wakifuatilia agenda jana mjini Sumbawanga .

(Habari na Picha na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa

………………………………………………………..

Na. OMM Rukwa

Serikali imeshauriwa kutoa elimu kwa wananchi hususan wanaoishi kwenye maeneo ya vyanzo vya maji na mabondeni endapo wanastahili kupatiwa anwani za makazi na postikodi.

Ushauri huo umetolewa na mwakilishi wa shirika la Sumango Vincent Kuligi wakati akichangia mada ihusuyo umuhimu wa zoezi la utambuzi makazi na uwekaji posticodi kwenye kikao cha Kamati ya Ushauri Mkoa wa Rukwa jana (01.03.2022) mjini Sumbawanga.

“Kuna watu wamejenga katika vyanzo vya maji. Je watahamishwa kabla ya kupata anwani za makazi au watapewa namba za nyumba huko huko wakati wa zoezi hili hapa kwetu Sumbawanga?” alihoji mwananchi huyo Vincent.

Akitoa ufafanuzi wa hoja hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti alisema lengo la serikali ni kutambua uhai wa watu wake ikiwemo kujua mahala gani wanaishi hivyo utambuzi wa makazi yao utafanyika licha ya kuwa wanaishi mabondeni.

Mkirikiti aliongeza kusema wataalam wa utambuzi wa anwani za makazi watafika maeneo yote ambako watu wanaishi na kuwaingiza kwenye regista ikiwemo nyumba zao ambapo alitoa wito kwa taasisi za Tanroad, Tarura na Shirika la Posta kushirikiana na halmashauri katika zoezi hilo.

“Kwa walio mabondeni na maeneo yaliyozuiwa tutawahesabu huko huko kisha kuwaeleza endapo wanaostahili au la kuishi maeneo hayo kwa mujibu wa sheria za nchi” alisema Mkirikiti.

Mkuu huyo alisisitiza na kutoa wito kwa viongozi wa vitongoji, vijiji, kata na wilaya kuwaelimisha wananchi juu ya kushiriki kwenye zoezi la utambuzi wa makazi na uwekaji anwani ili maandalizi ya sensa ya watu na makazi ya mwezi Agosti mwaka huu ifanikiwe.

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Tehama Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa Jonas Kilima Akiwasilisha mada juu ya maandalizi ya utekelezaji wa mfumo wa uwekaji anwani za makazi na postikodi alisema halmashauri zote nne zimeanza kutekeleza maelekezo ya serikali.

Aidha, Kilima alisema uhamasishaji jamii kuhusu zoezi hilo ikiwemo utambuzi wa majina ya barabara na mitaa pamoja na makazi imeanza katika halmashauri za Manispaa ya Sumbawanga, Sumbawanga DC, Nkasi DC na Kalambo.

Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Rukwa Rainer Lukala akizungumza kwenye kikao hicho aliahidi kuendelea kutoa elimu kwa wananchi ili agenda hiyo ya anwani za makazi ifanikiwe ikiwa ni sehemu ya utekelezaji ilani ya Uchaguzi wa Chama cha Mapinduzi.

Msingi wa kutekeleza Mfumo huu, ni ilani ya Chama cha Mapinduzi (2020-2025) kwamba ifikapo 2025 wananchi wote wawe na Anwani za Makazi pia ni utekelezaji wa maelekezo ya Sera ya Posta ya mwaka 2003.

Mwisho.

Previous articleDC SERERA AKABIDHI CHAKULA KWA WANAFUNZI SIMANJIRO
Next articleMO DEWJ ATOA POLE KWA GSM

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here