Featured Kitaifa

BILIONI 27 ZATOLEWA KUBORESHA BARABARA ZA RUKWA- RC MKIRIKITI

Written by mzalendoeditor

Mwenyekiti wa Bodi ya Barabara na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti ( aliyeshika kipaza sauti) akifungua kikao hicho leo mjini Sumbawanga. Wengine Kulia ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa Rainer Lukala. Kushoto wa kwanza ni Mbunge wa Kalambo Josephat Kandege akifuatiwa na Kaimu Katibu Tawala Mkoa Dkt. Boniface Kasululu.

Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Peter Lijuakali akifuatlia majadiliano leo kwenye kikao cha Bodi ya Barabara mkoa wa Rukwa kinachofanyika mjini Sumbawanga.

Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Dkt. Boniface Kasululu akizungumza leo kwenye kikao cha Bodi ya Barabara cha Mkoa wa Rukwa kilichofanyika leo mjini Sumbawanga.

Mbunge wa Nkasi Kaskazini Aida Khenani akizungumza kwenye kikao cha Barabara leo mjini Sumbawanga ambapo ameshauri Tanroad kutekeleza maazimio ya kikao kwa kujenga barabara kulingana na vipaumbele vilivyopitishwa na kikao.

Sehemu ya Wajumbe wa kikao cha Bodi ya Barabara Mkoa wa Rukwa wakiendelea kufuatilia agenda za kikao hicho leo mjini Sumbawanga.

…………………………

Na. OMM Rukwa.

Zaidi ya shilingi Bilioni 27.5 zimetolewa kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa barabara zilizo chini ya Wakala za TANROADS na TARURA katika mwaka wa fedha 2021/2022 ikiwa ni ongezeko la kibajeti mara mbili zaidi ya lile la awali kwa mwaka fedha uliopita.

Kutolewa kwa fedha hizo kunatajwa kuwa ni moja ya mafanikio makubwa ya serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan tangia aingie madaraka takribani mwaka mmoja hadi sasa.

Akizungumza katika ufunguzi wa kikao cha 40 Bodi ya Barabara mkoa hii leo (28.02.2022) mjini Sumbawanga, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti amesema fedha hizo tayari zinaendelea kutekeleza miradi ya barabara kwenye maeneo mbalimbali mkoani humo.

“Nichukue fursa hii kuipongeza serikali yetu inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutupatia fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya barabara zetu ambapo maendeleo makubwa yanaonekana kote “alisema Mkirikiti.

Mkuu huo wa Mkoa aliongeza kusema kqti ya fedha hizo shilingi Bilioni 15.2 ni kwa ajili ya barabara za Tanroads na Bilioni 12.3 ni kwa ajili ya barabara za Tarura.

Mkirikiti aliwataka wajumbe wa kikao hicho kufanya tathmini ya kina juu ya matumizi ya fedha hizo za barabara kwa kuwa zimetolewa na serikali kwa lengo la kuboresha barabara hususan za vijijini ili zichochee ukuaji wa uchumi .

“Fedha hizi ni zaidi ya mara tatu ya makusanyo ya halmashauri zetu zote nne. Makusanyo ya ndani ya halmashauri zetu ni Bilioni takribani 9 katika mwaka 2021/22” alisema Mkirikiti.

Aidha, Mbunge wa Kalambo Josephat Kandege aliomba serikali kufanya udhibiti na kulinda eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa uwanja mpya wa ndege Kisumba ili wananchi wasilivamie na kwa kilimo na makazi.

Akiwasilisha  taarifa ya utekelezaji kazi za barabara kuu za mkoa kwa mwaka 2021/22 na mpango na bajeti kwa mwaka 2022/2023 Meneja wa Tanroad Mkoa wa Rukwa Mhandisi Mgeni Mwanga alisema asilimia kubwa barabara za mkoa za lami na changarawe zote zilikuwa na hali nzuri.

Mhandisi  Mwanga  alisema Tanroad inasimamia mtandao wa barabara zenye urefu wa kilometa 1,250.2 ambapo barabara kuu zina urefu wa kilometa 415 kati ya hizo za lami ni (298.35 km) na changarawe (117.51 km) na  barabara za mkoa  zina jumla ya kilometa 834.98 kati hizo za lami ni (76.8 km) na za changarawe ni (758.1 km) .

Mhandisi Mwanga alisema katika mwaka 2022/2023 bajeti ya matengenezo kupitia Mfuko wa Barabara inayotarajia kupitishwa na Bunge ni shilingi Bilioni 13.81 ambapo jumla ya madaraja 32 katika barabara kuu na madaraja 62 katika barabara za mkoa yatajengwa na kukarabatiwa.

“Barabara nyingi zaidi zitajengwa na kufanyiwa matengenezo katika mwaka 2022/23 kuliko miaka iliyopitya na kuisaidia kuinua uchumi wa mkoa” alisisitiza Mhandisi Mwanga.

Naye Meneja wa Tarura Mkoa wa Rukwa Mhandisi  Seth Mwakyembe alisema wakala huo unahudumia mtandao wa barabara wenye urefu wa kilometa 2,304.6 kwenye halmashauri zote za Manispaa Sumbawanga (476.34 km), Sumbawanga DC (591.39 km), Nkasi DC (675.25 km) na Kalambo DC  (561.28 km).

“Tunapenda kuishukuru serikali kwa kuendelea kubuni vyanzo vipya vya mapato vinavyoiwezesha Tarura kutekeleza majukumu yao vema ambapo tayari serikali imetoa Bilioni 12 zinaendelea kutumika katika mwaka 2021/2022” alisema Mhandisi Mwakyembe.

Akichangi katika kikao hicho Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Rukwa Daniel Ntera alitoa ushauri kwa TARURA na TANROAD kuacha kutoa kazi kwa wakandarasi wasio na uwezo li kazi za ujenzi barabara uende kwa kasi na ubora.

Ntera aliongeza kusema changamoto nyingine iliyopo mkoa wa Rukwa ni kwa wahandisi wa TARURA wa wilaya za Nkasi na Kalambo kutofuatiliana na kusimamia kikamilifu miradi ya barabara.

“Mkandarasi mmoja kupewa kazi nyingi kwa wakati mmoja wakati uwezo wake ni mdogo hakipaswi kiendelee kwani kinachelewesha utekelezaji wa miradi hivyo ni vema kazi zitolewe kwa wenye uwezo” alisema Ntera.

Mbunge wa Sumbawanga Mjini Aishi Hilaly alitoa ushauri kwa viongozi wenzake kuacha kuomba kazi za ujenzi wa barabara ndani ya mkoa wa Rukwa ili kuwezesha watendaji kuwa na usimamizi mzuri.

“Tuna viongozi wanaomba kazi ndani ya Rukwa hatua inayokwamisha watendaji kufanya usimamizi wa barabara.Nashauri sisi tukaombe nje ya Rukwa” alisema Aeshi.

About the author

mzalendoeditor