Featured Kitaifa

NAIBU WAZIRI WA AFYA ATAKA KASI UJENZI WA MIUNDOMBINU YA AFYA MANYARA

Written by mzalendoeditor

Na Englibert Kayombo, WAF – Manyara.

Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel ameutaka Uongozi wa Afya Mkoa wa Manyara kuongeza kasi ya ujenzi wa miundombinu ya afya na kuikamilisha ndani ya wakati ili wananchi waweze kupata huduma.

Dkt. Mollel amesema hayo mara baada ya kufanya ziara katika Mkoa wa Manyara na kutembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara pamoja na Hospitali ya Wilaya ya Babati-Mrara na kukuta kasi ndogo ya ujenzi wa miundombinu.

“Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imekuwa ikileta fedha nyingi za miradi ya maendeleo katika Mkoa huu lakini kasi ya ujenzi wa miundombinu ya afya bado iko chini sana ukilinganisha na muda tulijiwekea kwa ajili ya kukamilisha miradi hiyo” amesema Dkt. Mollel.

Dkt. Mollel amesema Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara imepokea zaidi ya Shilingi Bilioni 3.6 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje, jengo la magonjwa ya dharura, Damu Salama pamoja Jengo la Wagonjwa mahututi lakini kasi ya ujenzi bado haridhishi.

“Tumeenda Hospitali ya Wilaya ya Babati (Mrara) ambayo imepokea Shilingi Milioni 300 kwa ajili ya ujenzi wa ‘Emergency Department’ pamoja na Shilingi Milioni 90 kwa ajili ya nyumba ya watumishi toka Mwezi Novemba 2021 lakini mpaka sasa hakuna kilichofanyika.

Kufuatia hali hiyo Dkt. Mollel amesema atarudi Mkoa wa Manyara baada ya wiki mbili kuangalia nini kimeanza kufanyika na kuutaka Uongozi wa Hospitali ya Wilaya ya Babati (Mrara) kuhakikisha wanaanza haraka ujenzi wa jengo la magonjwa ya dharura (Emergency Department) pamoja na nyumba ya watumishi.

“Hapa Manyara kuna kasi ndogo ya ujenzi wa miundombinu ya afya, nitarudi tena baada ya wiki mbili kuja kuona nini kilichoanza kufanyika, kama watendaji hawawezi hii kazi watupishe waje wenye uchungu na hii nchi kukamilisha hii miradi ili Watanzania waweze kupata huduma bora” Amesema Dkt. Mollel

About the author

mzalendoeditor