Featured Kitaifa

DKT.SHEIN AZINDUA ZOEZI LA UGAWAJI WA KADI ZA KIELEKTRONIKI MKOA WA KASKAZINI UNGUJA.

Written by mzalendoeditor

MAKAMU Mwenyekiti wa CCM Zanzibar ambaye pia ni Rais mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein akigawa kadi za CCM za  Kielektroniki wanachama mbalimbali wa Mkoa wa Kaskazini Unguja.

********************

NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein amewataka wanachama wa CCM kutofanya makosa ya kuwachagua viongozi wa chama kwa misingi ya ubaguzi  katika uchaguzi wa ndani unaotarajia kufanyika mwaka huu.  

Dk.Shein amesema wanachama wa CCM hawatakiwi kufanya makosa yakuchaguana katika uchaguzi huo kwa kubaguana kwa majina na badala yake wanatakiwa kuwachagua viongozi kwa kuzingatia uwezo na sifa.

Kauli hiyo ameitoa  wakati akizindua ugawaji wa kadi mpya za CCM za kieletroniki mkoa wa Kaskazini Unguja ambapo alisema kuna haja ya kuhakikisha viongozi hao wanachaguliwa kwa kuzingatia sifa za uwezo wa utendaji na ukereketwa wa CCM kwa kuifahamu chama na misingi yake.

“Tujitahidi sana katika uchaguzi huu kuwa wa aminifu na wakweli tusiwe wababahishaji hasa kwa kuwatumikia watu sisi tunatasimamia maadili chama hichi kina historia ya misingi ya usawa na haki ya kuwatumikia watu,”alisema

Dk.Shein alisema kuna kazi kubwa mbele ya safari kwa kuwapata viongozi watakaongoza miaka mitano ijayo hivyo kuna haja ya kuwachagua watu ambao wapo tayari kukitumikia chama.

“Katika jambo hili nafikiria watu hawa tunawajua katika matawi yetu tuna wajua kwa upande wa wilaya tunajuana hata kwenye mkoa hivyo tusiwaweke watu wenye tabia ya kutumatuma hatumii muda kukitumikia CCM,”alisema

Dk.Shein alisema mabadiliko yanayotokea duniani ndio imeifanya CCM kuanza kutumia mfumo wa Teknolojia za Habari na Mawasiliano(TEHAMA) pamoja na kadi mpya za kieletroniki.

Alisema mfumo wa TEHAMA una mafanikio makubwa zaidi pamoja na umadhubuti wake na kwamba kuna haja ya kuanza kuingia kwenye mfumo huo ikiwemo matumizi ya kadi za kietroniki.

Makamu huyo Mwenyekiti wa alisema matumizi ya mfumo wa TEHAMA una faida kubwa ambapo taarifa za mwanachama zitaweza kubakia hata kama kadi yake ameipoteza.

“Tunatarajia kutoa kadi hizi mpya ili kupata wanachama zaidi na pia ili demokrasia ndani ya chama ikue hivyo chama makini kama CCM lazima kiwe na uhai kila siku kwa kupata wanachama wapya hata hivyo tunapaswa kusimamia misingi ya demokrasia,”alisema

Alisema misingi hiyo ya demokrasia ni pamoja na kuhakikisha inasimamia makusanyo zaidi ya mapato ndani ya chama kuwatumikia wananchi na  ufanyaji wa kazi kwa usanifu.

“Wapo wanaofikiria kuwa siku hizi CCM hatujitegemea bado sisi tunategemea na tuendelee kujitegemea mambo mbalimbali tumeweza hivyo kujitegemea ni jukumu letu tangu ASP na TANU,”alisema

Dk.Shein alisema wanachama wa CCM wanapaswa kuunga mkono serikali mbili kutokana na kuwa chama kinaongoza serikali hizo ikiwemo serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Tuunge mkono jitihada za serikali zetu kila hatua kutokana na kuwa zinaongozwa na CCM kuna watu wanafanya utani mfano suala la uchumi wa buluu ni sera ya CCM na ipo ndani ya ilani ya chama hivyo lazima tuunge mkono sote,”alisema

Alisema wanachama wanapaswa kutambua kuwa haiwezekani hukajeli jambo lako na kwamba wanachama wanatakiwa kuwa pamoja na kwenda pamoja katika kila hatua.

Kwa upande wake Mjumbe Mstaafu wa Kamati Maalum na Makamu wa Pili wa Rais Mstaafu Balozi Seif Ali Idd alisema kadi mpya za CCM za kietroniki ni nzuri kutokana na kuwa ni rahisi kutunzika.

“Katika uchaguzi huu wanachama mnatakiwa kuhakikisha mnachagua watu wenye uwezo wa kufanya kazi na si kutumikia matumbo yao kwa kufanya kazi kwa ushirikiano na upendo mkubwa ili kufanikisha dira za CCM,” alisema

Alisema kazi ambazo zinafanywa na serikali ya awamu ya nane ni nzuri na kwamba inaonyesha matumahini makubwa ya kuiona Zanzibar itakuja kuwa kubwa kutokana na utendaji wa kazi zinazofanywa kwa uweledi mkubwa.

About the author

mzalendoeditor