Featured Michezo

WAZIRI MCHENGERWA ATEMBELEA MAONESHO YA DUBAI EXPO

Written by mzalendoeditor

Na. John Mapepele

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Mohamed Mchengerwa ametembelea banda la Tanzania katika Maonesho ya EXPO Dubai 2020 yanayoendelea katika Umoja wa Nchi za Falme za Kiarabu na kupongeza waoneshaji baada ya kujionea jinsi Tanzania inavyotumia maonesho hayo ya Kitamaifa kujitangaza.

Mhe, Mchengerwa. jana Februari 24, 2022 amepita kukagua kwenye mabanda hayo ya maonesho na kuhimiza utoaji wa maelezo kiufasaha ili wageni wanaotembelea mabanda hayo watambue vivutio mbalimbali vya utalii vinavyopatikana nchini hatimaye wafike kutembelea Tanzania.

Katika mabanda hayo, Tanzania inajitangaza kupitia fursa mbalimbali za Utalii, Madini, Nishati, Kilimo na Uwekezaji kwa wageni.

Mbali na maonesho ya kuonesha fursa mbalimbali pia Tanzania kwa mara ya kwanza imeutambulisha Utamaduni wa Tanzania kupitia muziki wa singeli duniani katika maonesho haya kupitia mfalme wa singeli nchini Sholo Mwamba ambaye amewachezesha singeli wageni kutoka maeneo mbalimbali duniani wakati alipopanda jukwaani jana Februari 24, 2022 kwenye ukumbi wa Earth Stage jijini Dubai.

Mbali ya Sholo Mwamba, pia Kikosi cha Mrisho Mpoto na msanii Saraphina tayari wametumbuiza katika maonesho hayo ya Dubai kwa mafanikio makubwa.

Katibu Mkuu wa Utamaduni, Sanaa na Muchezo. Dkt, Hassan Abbasi amesema kuwa Tanzania imeandika historia ya kuitambulisha Utamaduni wake kupitia muziki wa Singeli.

Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Sanaa nchini Dkt. Emmanuel Ishengoma amesema bado wasanii hao watapanda kesho majukwani kuendelea kuonesha Sanaa na Utamaduni wa Tanzania kupitia muziki.

About the author

mzalendoeditor