HALMASHAURI ya Bahi Mkoani Dodoma imeweka mikakati ya kuongeza ufaulu katika mitihani ya shule za msingi na sekondari ili kuwezesha kuingia kwenye kumi bora Kitaifa.

Akizungumza katika hafla ya utoaji tuzo kwa shule, walimu na wanafunzi waliofanya vizuri katika mtihani wa kumaliza elimu ya msingi na sekodari 2021,Mkuu wa Wilaya hiyo Mwanahamisi Munkunda amehimiza ushirikiano baina ya viongozi,walimu,wazazi na wanafunzi.

“Nikiangalia mtiririko wa ufaulu mwaka hadi mwaka tunaenda vizuri,lakini sasa tumeamua tuwe kwenye kumi bora, na hili litawezekana tukizidi kushirikiana,”

Ili kufanikisha hilo ametoa ombi kwa madiwani wa halmashauri hiyo,“Tunapoanza makambi niwaombe kila dawani asaidie debe moja la mahindi na maharage,”alisema.

Akitaja baadhi ya mikakati hiyo Afisa Elimu Msingi Boniface Wilson  amesema wanafunzi watapewa mitihani ya kutosha na tathimini ya kina kwa kila somo ili kubaini mapungufu,kupanda na kushuka kwa ufaulu na kubaini masomo ambayo wanafunzi hawafanyi vizuri. 

Alisema kwa darasa la saba kuanzia Disemba 2021 hadi Machi 2022,mitihani ya wilaya itafanyika mara moja kwa mwezi na kuanzia April 2022 hadi Juni 2022 mitihani itafanyika mara mbili kwa mwezi.

“Kuanzia Julai 2022 hadi Disemba 2022 mitihani itafanyika mara tatu kwa mwezi na kila shule ihakikishe inatoa mitihani kila wiki kwa madarasa ya mitihani pamoja na kufanya usahihi wa kina na kutunza alama,”alisema.

Kwa upande wake afisa elimu sekondari Marry Chakupewa amesema wamejipanga kufanya vikao vya tathmini kila mwezi ili kubaini changamoto na kuzitafutia ufumbuzi ikiwa ni pamoja na kutoa ushauri.

 “Tunahimiza pia ufundishaji wa vipindi vya ziada shuleni hasa kwa madarasa ya mitihani kwa kuhakikisha kila shule inakuwa na ratiba rekebishi na kufanya vikao na wazazi mwezi Januari kwa ajili ya kuweka mpango wa kuwapatia wanafunzi chakula cha mchana shuleni,”alisema.

Ili kufanikisha jitihada hizo ametoa mapendekezo kwa mamlaka zinazohusika kuchukua hatua za kisheria na kinidhamu kwa watuhumiwa, wazazi na viongozi wanaoshiriki kuwaficha wanaowapa mimba wanafunzi au kuwatorosha watuhumiwa.

Katika Halmashauri ya Wilaya ya Bahi kumekuwa na ongezeko la ufaulu kutoka asilimia 95 mwaka 2020 hadi asilimia  96 mwaka 2021 na kwak idato cha nne ufaulu umeongezeka kutoka asilimia 91.5 mwaka 2020 hadi asilimia 94 kwa mwaka 2021.

Upande wa elimu msingi ufaulu umekuwa ukiongezeka kila mwaka ambapo mwaka 2019 ulikuwa asilimia 78.84,mwaka 2020 asilimia 84.64  na mwaka 2021 ulifikia asilimia 92.4 na hivyo kufanya kuwemo kwenye halmashauri 10 zilizoboresha ufaulu kwa kiwango cha juu kitaifa.

Previous article‘SERIKALI YAFANIKIWA KUBORESHA ELIMU RUKWA’: RC MKIRIKITI
Next articleMADIWANI BAHI WAPAZA SAUTI MFUKO WA ELIMU

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here