Featured Kitaifa

MADIWANI BAHI WAPAZA SAUTI MFUKO WA ELIMU

Written by mzalendoeditor

BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Bahi Mkoani Dodoma limeielekeza Halmashauri hiyo kuingiza Sh Mil 50 kwenye mfuko wa Elimu Ili kutimiza utaratibu walioupitisha ndani ya kikao wa kuwa na mfuko utakaowasaidia wanafunzi wasiojiweza ambao wamefaulu kuendelea na masomo ya sekondari.

Akizungumza jana katika kikao cha mapitio ya utekelezaji wa bajeti 2020/2021 na mapitio ya nusu mwaka2020/2021 kilichofanyika wilayani humo,Mwenyekiti wa Halmashauri Donald Mejitii ambaye ni diwani wa Kata ya Lamaiti alisema uamuzi huo umefikiwa baada ya mfuko kuwa na Sh Milioni 10 tu hadi sasa.

“Huu mfuko tuliuanzisha kwa dhamira njema kabisa usaidie mahitaji kwa wanafunzi wetu wanaofaulu na hawana uwezo,na ili kulifanikisha hili tuliamua kwenye baraza kuongeza ushuru wa ng’ombe kutoka Sh 2,000 hadi 4,000 ili nyongeza hiyo iingie kwenye mfuko lakini utekelezaji wake umekuwa ukisuasua,”alisema.

Diwani wa Kata ya Ibugule Blandina Magawa alisema ucheleweshaji wa fedha katika mfuko huo kunapelekea wanafunzi kushindwa kuripoti shuleni kwa wakati kutokana na kukosa mahitaji kama sare za shule, madaftari,viatu na pesa za kujikimu kwa wanafunzi waliochaguliwa shule za bweni.

Mwenyekiti wa Kamati ya Elimu,Afya na Maji Sostenes Mpandu alisema dhamira njema ya serikali ya kujenga madarasa,kuajiri walimu haitaweza kuleta matokeo chanya kama watashindwa kuendeleza utaratibu ambao wao wenyewe wameuweka.

Akizungumza baada ya kupokea hoja hizo,Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Athumani Masasi aliahidi hadi mwezi wa tatu kiasi hicho cha fedha kitakuwa kwenye akaunti ya mfuko na watoto wote wanufaika watapata mahitaji yao.

“Nikiri sikuwa nimepata suala hili kwa haraka kujua utaratibu wake umekaaje,niiombe kamati ya Elimu ikutane Jumatatu kupitia majina ya walengwa na idadi itakayopatikana waanze kupewa mahitaji yao,na hapa niwaahidi katika makusanyo ya mapato ajenda ya kwanza itakuwa watoto kwenda shule,”alisisitiza.

Akihitimisha hoja hiyo Mkuu wa Wilaya ya Bahi Mwanahamisi Munkunda alielekeza fedha hizo kutolewa haraka ili watoto waende shule.

“Fedha hizi zimechelewa sana kutolewa,na ndio maana kwenye mahudhurio tunaona kuna watoto zaidi ya 1,000 hawapo shuleni na inawezekana sababu mojawapo ni kukosa mahitaji kwa watoto ambao wazazi wao hawana uwezo,”alisema.

About the author

mzalendoeditor