Featured Kitaifa

MWELEKEO MPYA WA ELIMU 2022/23 HUU HAPA

Written by mzalendoeditor

Na.Alex Sonna

Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Eliamani Sedoyeka  amewataka Makamu Wakuu wa Vyuo Vikuu vya Umma na Taasisi zilizo chini ya Wizara zinazotoa mafunzo kuweka mkazo kwenye elimu ya ufundi na ubunifu.

Prof.Sedoyeka ameyasema hayo  alipokutana na viongozi hao katika kikao cha kujadili mwelekeo wa bajeti ya 2022/23 kilichofanyika katika  Chuo cha Ufundi Arusha mkoani Arusha.

Prof. Sedoyeka alisema kikao hicho kinalenga kuangalia pia  kwa pamoja  mtazamo na mwelekeo wa nchi wa kuwa na uchumi wa viwanda, hivyo Sekta ya Elimu ina wajibu wa kuandaa vijana wenye  ujuzi wa kujiajiri na kuajiri wengine

Prof. Sedoyeka ameendelea kuelezea kuwa ili kufikia azma hiyo Vyuo vya Elimu ya Juu ni lazima kuanza kufikiria namna ya  kuanzisha viwanda (_Teaching_ Factories)  vitakavyowezesha  wanafunzi kujifunza kwa vitendo na kuzalisha fedha kwa ajili Vyuo.

“Katika kipindi hiki ambacho taasisi zinaandaa bajeti zake, malengo ya nchi kuelekea 2025 ni kuwa na nchi ya viwanda na Ilani ya Uchaguzi ya CCM inamuelekeza Rais mwelekeo wa nchi kwenda kwenye viwanda, wajibu wetu sekta ya elimu ni kutengeneza vijana wazalishaji wajakaojiari na kuajiri wenzao,”amesema.

Prof.Sedoyeka amesema “Katika vyuo vikuu tunakwenda dhana ya kuunda viwanda vya kufundishia ambapo itatengeneza mazingira ya wanafunzi kufanya kazi viwandani huku wakijifunza, kwa ujumla tumekubaliana kufanya hivyo, ambapo kila chuo katika mwaka 2022/23 kitatengeneza walau kiwanda kimoja chenye uwezo wa kuzalisha na kujiendesha kibiashara.”

Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ardhi, Prof.Evalisto Riwa, amesema hatua hiyo ni mwelekeo mpya wa wizara namna elimu inavyotakiwa.

Naye, Mwakilishi wa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Prof.Said Vuai, amesema dira ya Wizara ipo vyema na imelekeza zaidi namna Wizara inavyotaka kujiimarisha kwenye sayansi na teknolojia na kuchochea Tanzania ya viwanda.

About the author

mzalendoeditor