Featured Michezo

‘TUMETENGA BILIONI 19 KWA AJILI YA SHULE MAALUM 56 ZA MICHEZO’-WAZIRI BASHUNGWA

Written by mzalendoeditor

OR-TAMISEMI

Serikali imetenga Shule maalum 56 za Sekondari nchi nzima kwa ajili ya kukuza na kuendeleza vipaji mbalimbali vya michezo nchini vile vile kuanzisha shule za sekondari za kanda kwa ajili ya kuendeleza uboreshaji wa somo la elimu ya michezo nchini.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Innocent Bashungwa katika kikao kazi na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Mohamed Mchengerwa na viongozi wa Wizara zenye dhamana ya Elimu, Michezo na Ofisi ya Rais – TAMISEMI.

Waziri Bashungwa ameeleza kuwa uboreshaji wa miundombinu ya michezo na vifaa kwa ajili ya shule teule 56 za michezo utagharimu shilingi bilioni 19 na utaenda sambamba na kujenga shule za sekondari za kanda ambapo wanamichezo watakaopatikana katika shule hizo maalum wataweza kupatiwa nafasi ya kuendeleza vipaji na vipawa vyao katika shule hizo za kanda.

Aidha, Waziri Bashungwa ameeleza kuwa katika kikao hicho wamekubaliana na kupitisha mpango mkakati wa kusimamia utoaji wa elimu ya michezo katika shule za msingi na sekondari wa miaka mitano unaobainisha malengo, namna ya utekelezaji na matokeo ili utumike kama dira kwa kipindi cha muda mfupi na mrefu.

Kwa Upande wake, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema Wizara yake katika bajeti ijayo imejipanga kujenga viwanja vya kisasa ambapo wataanza na mikoa 10 vitakavyoenda samabamba na mpango wa kuboresha miundombinu na vifaa vya michezo katika shule teule 56.

Waziri Mchengerwa amesema kiu na ndoto ya Watanzania ni kushiriki na kufika kwenye ligi za kimataifa kwahiyo kilio chao ni kutokuwa na miundombinu ya michezo vilevile kutowaandaa Watanzania kushiriki katika michezo mbalimbali wakiwa bado katika maeneo ya chini kwenye msingi.

Chimbuko la kuanzishwa shule za michezo lilitokana na kukosekana kwa utaratibu maalum wa kuendeleza vipaji kwa wanamichezo chipukizi waliopo shuleni, Tanzania kushindwa kufanya vizuri katika Mashindano ya kimataifa licha ya kuwa na vipaji vingi na kuzorota kwa ufundishaji wa somo la michezo katika shule za msingi na sekondari.

About the author

mzalendoeditor