Featured Kitaifa

MABORESHO MAKUBWA ELIMU YA JUU KUFANYIKA

Written by mzalendoeditor

Na WyEST,DODOMA

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema katika kuendelea kuboresha Elimu ya Juu na kuongeza nafasi kupitia mradi wa “HEET” Serikali imepata mkopo nafuu wa takriban Shilingi bilioni 972 kutoka Benki ya Dunia.

Amesema hayo Jijini Dodoma Februari 12, 2022 katika mkutano maalum wa majadiliano kuhusu mafanikio katika Sekta ya Elimu katika kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan ulioendeshwa kupitia mtandao wa Zoom.

Ameeleza kuwa katika mwaka huu pia Serikali imeongeza bajeti ya fedha za mkopo wa Elimu ya Juu kutoka Shilingi bilioni 464 hadi kufikia bilioni 570 na hivyo kuwezesha Watanzania wengi zaidi kupata fursa ya kuendelea na masomo ya Elimu ya Juu.

“Tunataka pia wanafunzi wanaofanya vizuri katika masomo yao ya Elimu ya Juu waweze kupata skolashipu za kwenda kujiendeleza kielimu nje ya nchi ili kupata ujuzi zaidi katika fani wanazosomea,” ameongeza Prof. Mkenda.

Aidha, Mhe. Mkenda amesema Serikali katika kutambua umuhimu wa upatikanaji wa elimu kwa wote imejenga Shule ya Msingi Maalum Lukuledi, Mtwara na Shule ya Sekondari Maalum Patandi, Arusha ambazo ni Jumuishi zinazochukua wanafunzi wenye mahitaji maalum na kuwekeza katika vifaa vya kujifunzia na saidizi.

“Tumechapisha vitabu vya nukta nundu kwa ajili ya wanafunzi wasioona na tumenunua vishkwambi kwa ajili ya wanafunzi viziwi. Hii yote ni katika kuhakikisha watoto wote wa Kitanzania wanapata fursa sawa ya elimu,” amefafanua Mhe. Mkenda.

Waziri Mkenda ameongezea kuwa Wizara yake inaendelea na utekelezaji wa agizo la Mhe. Rais la kupitia mitaala ambapo tayari zoezi hilo limeshaanza kwa kuhusisha ukusanyaji maoni ya Wadau mbalimbali ikiwemo wanafunzi.

“Tutapitia pia Sera ya Elimu ya mwaka 2014 na Sheria ya Elimu sambamba na mchakato wa kuboresha mitaala ambao tayari tumeshauanza,” amesema Mhe. Mkenda.

Aidha, kuhusu elimu ya Ufundi Waziri Mkenda amesema Serikali inajenga Chuo kipya cha Ufundi Dodoma ambacho kitagharimu zaidi ya Shilingi bilioni 19 na kitakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 3,000 kikikamilika.

Amesema Serikali pia inajenga Vyuo vya VETA katika Wilaya 25 na vingine vinne katika mikoa ya Simiyu, Njombe, Rukwa na Geita.

Kuhusu Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDC) Mhe. Mkenda amesema Serikali imetenga jumla ya Shilingi bilioni 3.45 kwa ajili ya ukarabati na ununuzi wa samani kwa ajili ya vyuo hivyo.

Wadau mbalimbali walioshiriki katika Mkutano huo wamepongeza mafanikio katika Sekta ya Elimu na kutoa maoni yao ambayo yatasaidia kuendelea kuimarisha Sekta.

About the author

mzalendoeditor