Na Augusta Njoji, Handeni TC
HALMASHAURI ya Mji Handeni mkoani Tanga imetoa mikopo yenye thamani ya Sh. milioni 531.1 kwa vikundi 127 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kwa mwaka wa fedha 2024/25, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la serikali la kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya makundi hayo.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi hundi kwa vikundi hivyo, iliyofanyika Oktoba 25, 2025 mjini Handeni, Katibu Tawala wa Wilaya ya Handeni, Magreth Killo, akimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Mhe. Salum Nyamwese, amesema serikali imedhamiria kuwawezesha makundi hayo kujikwamua kiuchumi na kupunguza utegemezi katika jamii.
Amesisitiza kuwa uaminifu na uwazi ni nguzo muhimu katika utekelezaji wa miradi hiyo, akipiga marufuku tabia ya kutoa taarifa za uongo wakati wa kuomba au kukaguliwa kwa miradi.
“Udanganyifu unadhoofisha jitihada za serikali katika kujenga jamii yenye uadilifu. Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imeonyesha kwa vitendo dhamira ya kuwawezesha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kupitia mikopo isiyo na riba, elimu ya biashara na ujasiriamali, pamoja na mafunzo ya huduma bora ili mjikwamue kiuchumi,” amesema Kilo.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Handeni, Toba Mhina, amewataka wanufaika wa mikopo hiyo kuitumia kwa malengo yaliyokusudiwa na kuhakikisha wanarejesha kwa wakati ili vikundi vingine pia vinufaike.
Naye, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Fred Mpondachuma, amesema kuwa jumla ya vikundi 244 viliwasilisha maombi ya mikopo, na baada ya uchambuzi wa kina, vikundi 127 pekee ndivyo vilivyokidhi vigezo.
“Baadhi ya vikundi viliondolewa kwenye mpango huu kutokana na udanganyifu wa taarifa, ikiwemo kutoa taarifa za uongo kuhusu wanachama au miradi yao. Kwa mfano, kulikuwa na kikundi ambacho asilimia 80 ya wanachama wake hawakuwa wakazi wa Handeni bali wa wilaya nyingine,” amesema.
Mpondachuma ameongeza kuwa tangu mwaka 2017/2018, Halmashauri hiyo imetoa mikopo ya jumla ya Sh. milioni 953.6 kwa vikundi 304, vikundi vya wanawake 206, vijana 74, na watu wenye ulemavu 24 huku kiasi cha Sh.milioni 511.44, sawa na asilimia 54, kikiwa kimekwisharejeshwa.
Baadhi ya wanufaika wa mikopo hiyo wameishukuru serikali kwa jitihada hizo, wakieleza kuwa mikopo hiyo imewawezesha kuboresha biashara zao, kuongeza kipato na kubadilisha maisha yao kwa ujumla.
