Featured Kitaifa

MAJALIWA ATOA WIKI MOJA KITUO CHA POLISI NANDAGALA KIANZE HUDUMA

Written by Alex Sonna

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa leo Oktoba 23, 2025 amekagua ujenzi wa kituo cha Polisi Nandagala, Ruangwa mkoani Lindi na kuagiza kituo hicho kianze kazi ifikapo Novemba 1 mwaka huu.

Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa Frank Chonya kuhakikisha samani zinawekwa katika kituo hicho ili kiweze kutumika kwa kutoa huduma kwa Wakazi wa Wilaya ya Ruangwa.

“Wananchi hawa wanataka kituo hichi kianze kazi, majengo yamekamilika bado viti tu, hatuwezi kurudi kumdai IGP, Mkurugenzi simamia tupate viti hapa, pamoja na kuweka paving katika eneo hili, malengo yetu Novemba 1 mwaka huu kituo kianze kazi”

Kwa Upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, Kamishna Msaidizi wa Polisi, John Imori, amesema kuwa kiasi cha shilingi milioni 164 kilitengwa kwa ajili ya kujenga kituo cha Polisi cha daraja C, lakini Mheshimiwa Waziri Mkuu aliagiza kituo hicho kijengwe kwa mfumo wa force account na fedha nyingine zijenge nyumba za Maafisa wa Polisi.

“Tunakupongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, maagizo yako ya kujenga kwa mfumo wa force account yametuwezesha sasa tumepata na nyumba mbili za Maafisa wa Polisi, katika fedha ile milioni 164 tuliongeza shilingi milioni 30 tu hadi kukamilisha majengo haya matatu.”

Ujenzi wa kituo hicho ambao umegharimu kiasi cha shilingi milioni 194.3 umefikia asilimia 95 za utekelezaji, kukamilika kwake kutawezesha wananchi katika vijiji 32 kwenye kata 8 za Wilaya ya Ruangwa kupata huduma.

Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa alitembelea shule ya Sekondari ya Wasichana ya Liuguru ambapo aliwaeleza wanafunzi hao kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeongeza fursa kwa watoto wa kike kupata elimu nchini.

About the author

Alex Sonna