Mgombea ubunge wa Jimbo la Mtumba kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Anthony Mavunde, ameahidi kujenga kituo cha kukuza vipaji na michezo katika eneo la Sokoine, Ipala, ikiwa ni sehemu ya juhudi zake za kuendeleza vijana na kuhamasisha uwekezaji katika Kata ya Ipala.
Akizungumza wakati wa muendelezo wa kampeni zake katika kata hiyo, Mavunde amesema wananchi kwa muda mrefu wamekuwa wakitamani kuona miradi ya maendeleo na uwekezaji, na kwamba ameridhia ombi hilo kwa vitendo.
Amesema tayari wadau wengi wamejitokeza na kuonesha utayari wa kusaidia ujenzi wa miundombinu ya kituo hicho ikiwemo bwalo la watoto, litakalokuwa sehemu ya kituo hicho cha vipaji.
Mavunde ameongeza kuwa wanamichezo mashuhuri nchini, na nje ya nchi akiwemo Kocha Nasreddine Nabi, Miguel Gamondi,Skudu Makudubela,Aziz Ki,Feisal Salum “Fei Toto”, Aisha Masaka,Waziri Jr ,Zidane Boniface Pawasa,Edna Lema na Dickson Job, wameonesha utayari wa kumuunga mkono katika kuendeleza michezo na vipaji kwa vijana wa jimbo hilo.
Katika hatua nyingine, Mavunde amewahakikishia wananchi kuwa atakamilisha upimaji wa ardhi ili kila mkazi wa Ipala, Sokoine na Mwinyi aweze kumiliki hati miliki kwa urahisi.
Amesema atahakikisha kupitia Kliniki ya ardhi ofisi ya Idara ya Ardhi ya Jiji itahamishiwa katika eneo hilo ili kumaliza kabisa changamoto za muda mrefu za ardhi zinazowakabili wananchi.
Kuhusu changamoto ya maji, Mavunde amesema atahakikisha tatizo hilo linakwisha kwa kuchimba visima vyenye uwezo wa kuhudumia eneo lote la Ipala, akibainisha kuwa changamoto ya maji itabaki kuwa historia mara baada ya miradi hiyo kukamilika.
Ameeleza kuwa zahanati ya sasa imekuwa ndogo kutokana na ongezeko la watu katika kata hiyo, hivyo mwezi wa 11 baada ya kuapishwa, ataanza ujenzi wa kituo kipya cha afya kitakachotoa huduma bora na za uhakika kwa wananchi wa Ipala na maeneo jirani.