Featured Kitaifa

MHE. CHUMI APOKEA HATI ZA UTAMBILISHO MWAKILISHI WA WHO

Written by mzalendo

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Cosato Chumi amepokea Hati za Utambulisho za Mwakilishi Mkazi mpya wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dkt. Alex Gasasira.

Akimwakilisha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kupokea Hati hizo, Mhe. Naibu Waziri Chumi ameishukuru WHO kwa ushirikiano mzuri uliopo kati yake na Tanzania.

Mhe. Chumi ameeleza kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na WHO katika kuyafikia Malengo Endelevu ya Maendeleo 2030 (SDGs).

“Tanzania inapongeza juhudi za WHO katika kufikia lengo la Bilioni Tatu (Triple Billion) ambayo ni: watu bilioni moja kunufaika na Utoaji wa huduma bora za afya kwa wote, watu bilioni moja kulindwa vyema dhidi ya dharura za kiafya, na watu bilioni moja kufurahia afya bora na ustawi wa maisha,” amesema Mhe. Chumi.

Kwa upande wake Dkt. Gasasira ameishukuru Tanzania kwa kuwa mdau muhimu wa WHO akieleza kuwa WHo itaendelea kufanya kazi kwa karibu na Tanzania katika kuboresha mifumo ya afya na afya za Watanzania.

 

About the author

mzalendo